Mwanamke anaweza kufikwa na mambo yenye kusababisha damu ikatoka ukeni mwake. Mfano wa mambo hayo ni operesheni za kwenye tupu. Ziko aina mbili:

Ya kwanza: Anajua kuwa hatopata hedhi tena baada ya operesheni kwa sababu amefanya operesheni ya kuondosha tupu au ovari. Mwanamke huyu hana hukumu moja kama mwanamke mwenye damu ya ugonjwa; ana hukumu moja kama mwanamke mtwaharifu anayepata umanjano na maji ya uchafu-uchafu. Hivyo atatakiwa kuendelea kuswali, kufunga na kufanya jimaa. Hahitajii kuoga kwa ajili ya damu hii. Hata hivyo ni wajibu kwake kujiosha na kusitisha damu kwa kitambaa au kitu mfano wake ili damu isitoke. Kisha atawadhe kwa ajili ya swalah. Asitawadhe isipokuwa baada ya kuingia kwa wakati ikiwa kama swalah hiyo ina wakati maalum kama zile swalah tano. Vinginevyo, wakati wa swalah za sunnah zisizokuwa na nyakati maalum, atawadhe pale anapotaka.

Ya pili: Hajui kuwa hatopata hedhi baada ya operesheni; kuna uwezekano kabisa akapata hedhi. Mwanamke huyu ana hukumu moja kama mwanamke mwenye damu ya ugonjwa. Dalili ya hilo ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Faatwimah bint Abiy Hubaysh:

“Wakati hedhi inapokuja acha swalah. Pindi hedhi yako inapoisha jisafishe na uswali.”[1]

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Wakati hedhi inapokuja” inafahamisha kuwa hukumu ya damu ya ugonjwa inamhusu yule mwanamke ambaye anaweza kupata hedhi. Ama kuhusu mwanamke ambaye hawezi kupata hedhi, damu yake ni yenye kutoka kwenye mshipa uliyopasuka kwa hali yoyote ile.

[1] al-Bukhaariy (306).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016