19. Maswhabah hawakufasiri sifa za Allaah

78- Ama kuhusu maafikiano, Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wameafikiana juu ya kuacha kuzifasiri. Hali kadhalika watu wa kila karne walikuwa na msimamo huohuo. Tafsiri haikutoka kwa wengine isipokuwa kwa watu wa Bid´ah na watu walionasibishwa na Bid´ah.

79- Maafikiano ni hoja ya kukata kabisa. Kwani Allaah hawezi kuukusanya Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya upotevu. Maimamu baada yao wamesema waziwazi wakikataza kufasiri na kupindisha maana na wakaamrisha kuzipitisha Hadiyth hizi kama zilivyokuja. Tumenukuu maafikiano yao ndio maana ni wajibu kuwafuata na ni haramu kwenda kinyume nao.

Ima Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), makhaliyfah waongofu na Maswahabah walijua sifa zitafasiriwa au hawakujua. Kama hawakujua hilo, ni vipi walijua wale waliokuja baadaye? Hivi inawezekana kweli elimu hiyo ikawa ilifichikana kwao na wakaijua wanafalsafa kutokana na fadhilah zao?

80- Na kama walijua lakini wakanyamaza, basi ni lazima kwetu na sisi tunyamaze. Allaah asimrehemu yule asiyeweza kufanya kile walichofanya.

Kufasiri sifa za Allaah ima ikawa ni sehemu ya dini kwa njia ya kwamba haikamiliki isipokuwa kwa kupatikana jambo hilo au si sehemu yake. Ikiwa atapatikana mtu atakayesema kuwa ni sehemu ya dini, basi

“tutamuuliza iwapo Allaah alisema kweli pindi alisema kabla ya kujitokeza kwa upindishaji wa tafsiri:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

“Leo nimekukamilishieni dini yenu.”[1]

Au anamaanisha kwamba dini haikutimia mpaka pale alipoitimiza?

Ikiwa upindishaji wa tafsiri unaingia katika dini na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake wakawa hawakulikubali, basi dini yao ilikuwa pungufu tofauti na dini ya mwenye kufanya upindishaji huu. Haya hayasemwi na muislamu.

Na ikiwa upindishaji huu unaingia katika dini na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa hakuwafikishia Ummah wake, basi kwa hakika atakuwa amewafanyia khiyana na kuwaficha dini yao na hakutekeleza amri ya Mola Wake (Ta´ala) pale alipomwambia:

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ

“Ee Mtume! Fikisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako. Na usipofanya, basi utakuwa hukufikisha ujumbe Wake.”[2]

فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ

“Hivyo tangaza wazi yale uliyoamrishwa.”[3]

Kwa hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wale walioshuhudia kwamba amefikisha watakuwa sio wakweli – kufikiria hivo ni kumkufuru Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 05:03

[2] 05:67

[3] 15:94

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 19/12/2018