23- Inafaa kutangazia kifo cha maiti ikiwa utangazaji huo hautoambatana na Na´y ya kipindi cha kikafiri. Wakati fulani jambo hilo la kutangazaa linaweza kuwa la lazima ikiwa alipofia hakuna wawezao kumtekelezea haki yake ya kumuosha, kumvika sanda, kumswalia na mfano wa hayo. Kutokana na hayo kuna Hadiyth zifuatazo:

1- Abu Hurayrah ameeleza:

“Kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitangaza kifo cha an-Najaashiy katika siku aliyokufa ndani yake; alitoka kwenda mahali pa kuswalia, akawapangisha safu na akapiga Takbiyr nne.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim na wengineo. Ziada zake zote zitakuja kupitia njia zake mbalimbali katika masuala 60 katika Hadiyth ya saba.

2- Anas amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Zayd alikamata bendera ya vita akauawa. Kisha Ja´far alikamata bendera akauawa. Kisha akaishika ´Abdullaah bin Rawaah akauawa – macho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yakawa yanatokwa na machozi – Halafu bendera ikashikwa na Khaalid bin al-Waliyd pasi na uongozi aliyopewa wakapata nusura kupitia yeye.”

Ameipokea al-Bukhaariy na akaiwekea mlango na ile Hadiyth ilitoangulia kabla yake kwa kusema:

 “Mlango kuhusu mtu anayetoa taarifa za kifo kwa familia yake yeye mwenyewe.”

al-Haafidhw amesema:

“Faida ya mlango huu ni ishara kwamba si aina zote za Na´y kwamba zimekatazwa. Aina iliyokatazwa ni ile Na´y waliyokuwa wakiifanya watu wa kipindi cha kikafiri. Walikuwa wakimtuma mjumbe kutangaza kifo cha maiti kwenye milango ya nyumba na masokoni… “

Jambo hili likuwa limekubalika, basi itambulike kwamba kupiga makelele juu ya jambo hilo juu ya minara basi ni jambo lina haki zaidi liwe Na´y. Kwa ajili hiyo tumesema kwa njia ya kukata katika kipengele kilichotangulia kabla ya hichi. Huenda jambo hilo likaambatana na mambo mengine ambayo yenyewe kama yenyewe ni mambo mengine ya haramu. Kwa mfano kupokea malipo juu ya utangazaji huu wa kupiga makelele, kumsifia maiti kwa mambo yanayotambulika ni kinyume na hivo, kama pale wanaposema:

“Swalah juu ya watu watukufu waliokirimiwa na miongoni mwa Salaf wema wa mwishomwisho waliobaki… “

24- Imependekezwa kwa yule mtoa khabari kuwaomba watu wamuombee msamaha yule maiti. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilituma jesho la viongozi ambapo akasema: “Kiongozi wenu ni Zayd bin Haarith. Akiuawa basi apokee Ja´far bin Abiy Twaalib. Akiuawa basi apokee ´Abdullaah bin Rawaah al-Answaariy. Tahamaki Ja´far akaruka na kusema: “Namtoa fidia baba yangu na mama yangu, ee Mtume wa Allaah! Sikuwa mimi nikichelea kumfanya Zayd kuwa ni kiongozi juu yangu.” Akasema: “Lipitishe hilo! Hakika wewe hujui ni lipi katika hayo lina kheri.”  Wakaondoka na wakakaa muda aliotaka Allaah. Halafu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapanda juu ya mimbari na akaamrisha kutangazwe “Swalah iwakusanye!”. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Limepita jambo la kheri” au “Kheri zimekuwa nyingi” – Shaka kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan (bi maana Ibn Mahdiy). Je, nikukhabarisheni juu ya jeshi lenu hili linalopambana? Waliondoka na wakakutana na maadui. Zayd akauawa akiwa ni shahidi, muombeeni msamaha – ambapo watu wakamuombea msamaha. Kisha Ja´far bin Abiy Twaalib akakamata bendera na akajitahidi kupambana mpaka akauawa shahidi. Namshuhudilia kuwa amekufa shahidi. Hvyo muombeeni msamaha. Kisha akaishika ´Abdullaah bin Rawaah ikathibiti miguu yake mpaka akauawa akiwa ni shahidi. Hivyo muombeeni msamaha. Halafu bendera ikashikwa na Khaalid bin al-Waliyd – na hakuwa miongoni mwa wale viongozi, bali yeye mwenyewe ndiye alijifanya kiongozi – Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akainua vidole vyake viwili na kusema:

“Ee Allaah! Hakika yeye ni upanga miongoni mwa panga Zako. Hivyo mpe nusura.”

Kuanzia wakati huo Khaalid akaitwa “Upanga wa Allaah” (Sayfullaah). Kisha akasema: “Tokeni mwende mkawasaidie ndugu zenu na wala asibaki nyuma yeyote. Watu wakatoka kipindi cha joto kali hali ya kuwa (baadhi) wakitembelea na (wengine) wakiwa wamepanda vipando.”

Ameipokea Ahmad (05/299, 300-301) na kwa cheni ya wapokezi nzuri.

Kuhusiana na maudhui haya zipo Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah na wengineo juu ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ile siku alipotangaza kwa watu kuhusu kifo cha an-Najaashiy aliposema:

“Muombeeni msamaha ndugu yenu.”

Yatakuja katika masuala ya 60 ukurasa wa 87-88[1].

[1] Miongoni mwa mambo tuliyotangulia kufunza ni kwamba maneno ya watu katika baadhi ya nchi:

”al-Faatihah juu ya roho ya fulani.”

ni jambo linalokwenda kinyume na Sunnah iliyotajwa. Hapana shaka kwamba ni kitendo cha Bid´ah na khaswa ukizingatia kwamba kisomo hakimfikii maiti kwa mujibu wa maoni yenye nguvu, kama ambavyo upambanuzi wake utakuja – Allaah (Ta´ala) akitaka.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 45-47
  • Imechapishwa: 08/01/2020