20. Anayeitakidi kuwa kuna yeyote ana haki ya kutoka katika Shari´ah ya Muhammad

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

09 – Mwenye kuitakidi kuwa kuna watu wana haki kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – kama ambavyo Khadhr alivyopata kutoka katika Shari´ah ya Muusa (´alayhis-Salaam) – ni kafiri.

MAELEZO

Mwenye kuitakidi kuwa kuna yeyote anaweza kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama jinsi Khadhr alivyopata kutoka katika Shari´ah ya Muusa, ni kafiri. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake; naye Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[1]

Hilo ni kwa sababu Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imeenea kwa viumbe wote wawili; majini na watu, waarabu na wasiokuwa waarabu. Jengine ni kwamba Shari´ah ya Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio ya mwisho kabisa na yenye kufuta Shari´ah nyingine zote. Allaah (Ta´ala) amesema:

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَىٰ عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe mwonyaji kwa walimwengu.”[2]

وَأَرْسَلْنَاكَ لِلنَّاسِ رَسُولًا ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا

“Tumekutuma kwa watu uwe Mtume na inatosheleza Allaah kuwa ni Mwenye kushuhudia yote.”[3]

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote”.”[4]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, hakuna yeyote katika Ummah huu atayesikia kuhusu mimi – ni mamoja awe ni myahudi au mnaswara – halafu asiniamini isipokuwa ataingia Motoni.”[5]

“Nimepewa vitano ambavyo hakupewa Mtume yoyote kabla yangu.” Moja wapo akataja: “Nabii alikuwa anatumwa kwa watu wake maalum na mimi nimetumwa kwa watu wote.”[6]

Kwa hivyo yule mwenye kuitakidi kuwa inajuzu kwa yeyote kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamwabudu Allaah kwa Shari´ah nyingine, basi ni kafiri. Kwa sababu Shari´ah ya Muhammad ni yenye kuenea; kwa majini na watu, waarabu na wasiokuwa waarabu. Aidha ni kwa sababu Shari´ah yake imefuta Shari´ah nyingine zote. Vilevile ni kwa sababu baada ya kutumwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Shari´ah yake ni yenye kumgusa kila aliyepo [katika ulimwengu huu] mpaka siku ya Qiyaamah. Hili ni tofauti na Shari´ah ya Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Shari´ah yake aliyokuja nayo haikuwa yenye kuwaenea watu wote. Shari´ah yake ilikuwa inawahusu tu wana wa Israa´iyl. Kwa ajili hii ndio maana Khadhr alipata kutoka katika Shari´ah ya Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Isitoshe mambo ni kwamba kwa mujibu wa maoni ni kuwa Khadhr ni Nabii anayeteremshiwa Wahy. Ndio maana Muusa akaja kujifunza kutoka kwake, kama jinsi Allaah alivyotuelezea hilo katika Suurah al-Kahf. Vilevile imethibiti katika Hadiyth ambayo ni Swahiyh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimama akitoa Khutbah kwa wana wa israaiyl ambapo akaulizwa: “Ni mtu gani mjuzi zaidi?” Akajibu: “Mimi ndiye mjuzi zaidi.” Allaah akamlaumu kwa vile hakuirudisha elimu Kwake na akamteremshia Wahy: “Nina mja wangu ambaye yuko pale ambapo yanapokutana maji ya bahari mbili ni mjuzi zaidi kuliko wewe.” Akasema: “Ee Mola wangu! Ni vipi nitamfikia?” Akaambiwa: “Mchukue samaki kwenye kikapu. Pale utapomkosa basi anapatikana hapo. Akaondoka yeye na kijana ambaye ni Yuushaa´ bin Nuun na wakamuweka samaki kwenye kikapu. Mpaka walipofika kwenye mwamba wakaweka vichwa vyao chini na kujipumzisha. Hapo ndipo samaki yule akaruka kutoka kwenye kikapu kila na kushika njia yake baharini akiponyoka chini kwa chini, kitendo ambacho kwa Muusa na kijana yule kilikuwa cha kushangaza. Wakaondoka sehemu iliyobaki ya muda wa usiku na mchana wao. Walipoamka asubuhi, lete chakula chetu, kwani hakika tumepata machofu ya kutosha katika safari yetu hii. Muusa hakupata uchovu kabisa mpaka pale alipofika yale maoneo alipoelekezwa. Kijana wake akawambia: “Unaona pale tulipopumzika kwenye mwamba. Basi mimi hapo ndipo nilimsahau samaki.” Basi Muusa akamwambia: “Hapo ndipo tulipokuwa tunapataka. Basi wakarudi nyuma kwa kufuata athari za nyayo zao.” Wakati walipofika katika mwamba, wakamkuta bwana mmoja ambaye alikuwa amefunikwa nguo. Muusa akamtolea salamu. Khadhir akasema: “Umejuaje salamu hii kwani katika ulimwengu wako kuna salamu?” Akasema: “Mimi ni Muusa wa wana wa israaiyl.” Akasema: “Ndio.” Muusa akasema: “Je, nikufuate ili unifunze katika yale uliyofunzwa ya busara?” Akasema: “Hakika hutoweza kustahamili pamoja nami. Ee Muusa! Hakika mimi ninayo elimu kutoka kwa Allaah (Ta´ala) ambayo amenifunza; huijui wewe. Na wewe uko na elimu kutoka kwa Allaah (Ta´ala) aliyokufunza ambayo siijui mimi.” Akasema: “Utanikuta – Allaah akitaka – kuwa ni mwenye subira na wala sitokuasi amri yako.” Basi wakaondoka hali ya kutembea kando na bahari. Walipokuwa wanaendelea na safari yao wakaipitia safina ambapo wakawaomba wawape lifti. Wakamtambua Khadhr na akawaacha waingie ndani bila malipo. Akaja ndege na akatua kwenye ukingo wa ile safina na akadonoa mara moja au mara mbili ndani ya bahari ile. Khadhr akasema: “Ee Muusa! Elimu yangu mimi na wewe ukilinganisha na elimu ya Allaah haikupunguza chochote isipokuwa kama mfano wa ndege huyu alivodonoa ndani ya bahari hii.” Basi tahamaki Khadhr akachukua mbao moja ya safina ile na kuing´oa.” Muusa akasema: “Hivi kweli watu waliotubeba pasi na malipo umekusudia kuitoboa ili uwazamishe watu wake?” Akasema: “Je, sikusema kwamba hakika wewe hutoweza kustahamili pamoja nami?” Akasema: “Usinichukulie kwa niliyoyasahau.” Mara ya kwanza ikawa Muusa ameuliza kwa kusahau. Wakaendelea na safari na tahamaki wakamkuta mtoto akicheza na wenzake. Khadhr akakishika kichwa chake kutoka kwa juu na akaking´oa kwa mkono wake. Muusa akasema: “Umeua mtu asiye na hatia na ambaye hakuua mtu?” Akasema: “Je, sikukwambia kuwa hakika wewe hutoweza kustahamili pamoja nami?”

Ibn ´Uyaynah akasema: “Mara hii ametilia mkazo zaidi.”

“Basi wakaendelea na safari yao mpaka mpaka wakawafikia watu wa mji, wakawaomba watu wake chakula lakini walikataa kuwakaribisha. Wakakuta humo ukuta unataka kuanguka ambapo Khadhr akausimamisha kuujenga kwa mikono yake. Muusa akasema: “Ungelitaka basi ungeliuchukulia malipo juu yake.” Akamwambia: “Huku ndiko kufarikiana baina yangu na baina yako.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amrehemu Muusa! Natamani laiti angelikuwa na subira ili tuzidi kupewa kisa kuhusu jambo lao.””[7]

[1] 03:85

[2] 25:01

[3] 04:79

[4] 07:158

[5] Muslim (153)

[6] al-Bukhaariy (335) na (438) na Muslim (521)

[7] al-Bukhaariy (122, 74, 78, 2267, 2728, 3278, 3400, 3401, 4725, 4727, 6672, 7478) na Muslim Muslim (2380).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 49-52
  • Imechapishwa: 15/04/2023