21. Sababu mbili za Khadhr kutofuata Shari´ah ya Muusa

Kwa hiyo Shari´ah ya Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haimlazimu Khadhr kwa sababu hakuwa ni katika wana wa israa´iyl. Yeye ni mwenye kutoka katika Shari´ah ya Muusa. Anayedai kuwa inajuzu kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama ilivyojuzu kwa Khadhr kutoka katika Shari´ah ya Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kafiri. Kwa sababu mbili zifuatazo:

1 – Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwa walimwengu wote ilihali Shari´ah ya Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwa watu maalum. Kwa hiyo Shari´ah ya Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haimlazimu Khadhr. Kuhusu sisi Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yenye kutulazimu.

2 – Kwa mujibu wa maoni sahihi ni kwamba Khadhr ni Nabii anayeteremshiwa Wahy. Kwa hiyo yeye anafuata Shari´ah yake kama ambavyo Muusa pia na yeye anafuata Shari´ah yake.

Mwenye kuamini kuwa ana haki yeye au mwingine ya kutofuata Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuabudu Allaah kwa mfumo mwingine isiyokuwa Shari´ah aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kafiri kwa maafikiano ya waislamu. Kwa sababu Shari´ah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yenye kuenea kwa viumbe viwili; majini na watu. Jengine ni kwa sababu hakushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.

Yule mwenye kusema kuwa Shari´ah ya Muhammad au utume Wake ni kwa watu maalum, ambao ni waarabu, akasema kuwa kuna Mtume mwingine baada yake, basi atakuwa hakushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah na hivyo anakuwa kafiri. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake, hakuna yeyote katika Ummah huu atayesikia kuhusu mimi – ni mamoja awe ni myahudi au mnaswara – halafu asiniamini isipokuwa ataingia Motoni.”

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 15/04/2023