16- Shaykh Hasan bin ´Abdil-Wahhaab al-Bannaa (Hafidhwahu Allaah)


Amesema (Waffaqahu Allaah):

“Kwa jina la Allaah, himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na salamu zimwendee Mtume wa Allaah, ahli zake na Maswahabah zake.

Amma ba´d:

Allaah alitaka Chuo Kikuu cha al-Madiynah an-Nabawiyyah kunitafuta ili kufundisha katika mwaka wa masomo 1391/1392 H mpaka 141405/1406 H. Kabla ya Chuo Kikuu kunichagua nilikuwa namjua muheshimiwa Shaykh Rabiy´ kupitia kaka yangu Shaykh Muhammad ´Abdul-Wahhaab al-Bannaa – ambaye ni mwenza wa Shaykh Rabiy´ katika kulingania katika ´Aqiydah Salafiyyah na kupambana na Bid´ah – Shaykh Rabiy´ alikuwa ametakharuji kwenye Chuo Kikuu cha Kiislamu, kisha akapata shahada yake ya pili na akaendelea kusoma ili kufika katika shahada ya udaktari na kipindi hicho alikuwa akihudhuria Cairo na akikutana na baadhi ya wanachuoni katika yale yanayohusiana na utafiti wake juu ya shahada yake ya pili.

Kisha Shaykh Rabiy´ akahamishwa kwenda Makkah al-Mukarramah ili kufuatilia masomo yake na utafiti wake – baina ya Makkah na al-Madiynah – chini ya usimamizi wa maprofesa wanaosimamia utafiti huo. Nilikuwa nikisafiri kwenda Makkah kwa ajili ya ´Umrah na nikiandamana na ndugu yangu kwa ajili ya kumtembelea Shaykh Rabiy´. Wakati fulani yeye ndiye alikuwa akitualika kwenda kumtembelea. Sehemu kubwa ya vikao vyake vilikuwa vinahusiana na elimu na khaswa elimu ya Hadiyth. Tulikuwa tukifaidika kwa mahojiano kati ya kaka yangu na wahudhuriaji pamoja na Shaykh Rabiy´ katika vikao hivi.

Kisha muheshimiwa Shaykh Rabiy´ Haadiy al-Madkhaliy akajiunga na Chuo Kikuu cha Kiislamu ili kufundisha ndani yake baada ya kufika kupata shahada ya udaktari. Alikuwa akifurahikia somo na kufundisha kwake. Kisha akatuliza makazi al-Madiynah kwa vile tulikuwa tukimtembelea na tukifaidika  kutoka katika elimu yake wakati tulipokuwa tukifundisha ´Aqiydah na elimu ya Kishari´ah kwenye Chuo Kikuu cha Kiislamu pamoja na Ustadhw  na rafiki yangu muheshimiwa Shaykh Dr. Sa´d ´Abd-ur-Rahmaan Nidaa´ ambaye ni profesa wa ´Aqiydah katika Chuo Kikuu cha Kiislamu ambaye alikuwa akijadiliana na Ahl-ul-Bid´ah na waliopinda kwenye ´Aqiydah katika waalimu wa Chuo Kikuu na wengine waliokuwa wakiishi al-Madiynah.

Muheshimiwa Shaykh Rabiy´ Haadiy al-Madkhaliy siku zote alikuwa na mafungamano yenye kudumu na wanachuoni katika Ahl-us-Sunnah na khaswakhaswa Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz na Shaykh Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy (Rahimahumaa Allaah) na wengineo. Alichukua kutoka katika elimu na mahojiano yao. Kisha akaanza kufuatilia maneno ya walinganizi walioko uwanjani na kuyapima maneno yao kwa misingi ya Ahl-us-Sunnah. Yule anayemuona kuwa amepatia basi anamsifu kwa yale anayostahiki – bila ya kumtakasa mbele ya Allaah – na yule anayemuona kutokana na ujuzi wake kuwa amekwenda kinyume na misingi ya Ahl-us-Sunnah basi anamnasihi. Akijirudi basi huyo ni ndugu yake na asipojirejea na akaendelea kueneza Bid´ah zake basi anamzungumza katika mazungumzo yake kwamba amekhalifu misingi katika kitu fulani na fulani na kwamba amemnasihi lakini hata hivyo hakujirudi ili wapate kujulikana wale Ahl-us-Sunnah wa asili kutokamana na wale walioko uchi na waweze kutengwa. Anafanya hivo kwa kuzingatia misingi ya elimu ya Jard na Ta´diyl. Kwani akiachwa mmoja wao juu ya makosa yake basi wengine watamfuata, ikiwa ni masuala yanayokwenda kinyume na misingi basi yataenea kwa wengine pia, wako ambao wataivamia baadhi ya misingi ya Ahl-us-Sunnah kuzidisha, kupunguza au kufafanua yale yaliyokuja kwa njia ya ujumla kwa njia ambayo haikufanywa na Salaf. Kila wamoja katika watu hawa ambao wanarejelewa katika makosa yao hukasirishwa na maneno yake [Shaykh Rabiy´] kwa sababu anafichua uchi wake mbele za watu na hivyo watu wakamjua kwa upungufu wake na pengine hata watu wakaachana naye. Haya khaswa ukizingatia kwamba baadhi ya wanachuoni wanamuona kuwa ni mkali katika haki, jambo ambalo ni sifa na sio kusimangwa.

Kuna ambao wamejaribu kumzuia Shaykh Rabiy´ kutothibiti juu ya haki, kuwanusuru watu wake, kuitetea dhidi ya kila mzushi na kupambana na misingi inayopingana na Ahl-us-Sunnah. Lakini hata hivyo Allaah amemfanya kuwa imara na hilo likamfanya kuwa na nguvu zaidi katika haki na kuendelea kushikamana na njia hii ambayo ndani yake inawafichua wazushi na njia zao za waziwazi na zilizojificha.

Mimi nashuhudia – pamoja na udhaifu wangu katika elimu ambao nataraji Allaah atauunga kwa kule kushikamana barabara na misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na yale matawi yanayoifuatia – ya kwamba muheshimiwa Shaykh Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy ni miongoni mwa wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah mwa marefu na mapana. Maneno yangu haya ni kwa ajili ya kumtambulisha ili wapatikane wabora kutoka katika Ummah huu, baada ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), wenye kuuelekeza na kuwashika mikono yao kuwaelekeza katika njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na Firqat-un-Naajiyah ili kupatikane umoja wa Ummah chini ya bendera ya Tawhiyd na Sunnah na hivyo upate utukufu na ushindi, ukusanye furaha ya duniani na Aakhirah.

Itambulike kuwa muheshimiwa Shaykh Muqbil bin Haadiy (Rahimahu Allaah) alikuwa akichota kutoka kwenye chemchem ileile aliyochukua Shaykh Rabiy´ bin Haadiy. Yeye ni katika wenzake. Wote wawili wanatambulika kwa ukali wao wenye kusifiwa dhidi ya wenye kwenda kinyume na misingi ya mfumo wa ki-Salafiy. Kadhalika Shaykh Muhammad ´Abdul-Wahhaab al-Bannaa – miongoni mwa waasisi wa kundi la Answaar-us-Sunnah al-Muhamadiyyah Misri na mkurugenzi wa mwongozo wa Kiislamu katika kurugenzi ya mafunzo Jeddah Saudi Arabia hapo kabla – ni miongoni mwa rika la Shaykh Rabiy´ ambaye alishirikiana naye katika kuinusuru Sunnah na kuitokomeza Bid´ah.

Hakika nimefaidika sana kutoka kwa Shaykh Rabiy´, nimejifunza kutoka katika vitabu vyake na inanitukuza kuwa mmoja katika wanafunzi wake.

Ni lazima kwa watu wote wakati wa mzozo kuhukumiana kwa Qur-aan na Sunnah kwa ufahamu wa wema walitoangulia. Sambamba na hilo waachane na ushabiki mbaya, kufuata kichwa mchunga na kuwa, jeuri dhidi ya haki na kuwachukia watu wake. Watu wapeane nasaha kwa njia iliokuwa nzuri zaidi na wakati huohuo kila mmoja athaminiwe thamani yake stahiki.

Haya machache niliyotaja yanashuhudilia mfumo wa Shaykh Rabiy´ pamoja na kuafikiana na madhehebu ya Ahl-us-Sunnah. Hayo yanapata kubainika kupitia vitabu vyake, duruus zake, mahojiano yake, mihadhara yake na tovuti yake ya Sahab.net

Yameandikwa na:

Hasan ´Abdul-Wahhaab al-Bannaa

Mjumbe wa Answaar-us-Sunnah al-Muhamadiyyah

Aliwahi kuwa mwalimu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Madiynah al-Munawwarah.

Aliwahi kuwa mjumbe wa mwamko wa Kiislamu al-Madiynah.

Usiku wa alkhamisi tarehe 30 Rabiy´ al-Awwal 1425 H

  • Mhusika: Shaykh Khaalid bin Dhwahwiy adh-Dhwafayriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.rabee.net/ar/sharticles.php?cat=12&id=57
  • Imechapishwa: 09/12/2019