70- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema: “Ni nani atayechukua maneno haya matano kutoka kwangu na kuyafanyia kazi au kumfunza nayo ambaye atayatendea kazi?” Nikasema: “Mimi, ewe Mtume wa Allaah.” Akachukua mkono wangu na kuhesabu mara tano: “Jiepushe na madhambi utakuwa mfanya ´ibaadah mkubwa. Ridhika na kile Allaah alichokupa utakuwa tajiri mkubwa. Mfanyie wema jirani yako utakuwa muumini mkubwa. Watamanie watu yale unayojitamania mwenyewe utakuwa muislamu. Usicheke sana. Vicheko vingi vinaufisha moyo.”[1]

71- Umm-ud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Nilimsikia Abud-Dardaa´ akisema: “Lau mtu angeliikimbia riziki yake kama anavyoyakimbia mauti basi ingelimuwahi kama jinsi mauti yanavyomuwahi.”

72- ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna riziki mbili; riziki inayokutafuta na riziki unayoitafuta.”

73- Baadhi ya wanachuoni wameifasiri kwa kusema:

“Riziki inayokutafuta ni kile chakula cha mchana na riziki unayoitafuta ni ile ya kupita kiasi.”

74- Ibn Haazim amesema:

“Nimekuta vitu vyote viko aina mbili; ambacho ni changu na cha mwengine. Kile ambacho ni changu nitakipata tu hata kama nitakiendea kwa mapambano makali, na kile ambacho si changu sintokipata hata kama sintokiendea kwa mapambano makali.”

75- Shifaa bin Maati´ amesema:

“Kuna mtu alikuwa na kipande cha mkate safarini. Akawa anatazama kipande cha mkate kile na akilia na kusema: “Nikikila nitakufa.” Ndipo Allaah akamtumia Malaika na kusema: “Akila kipande cha mkate kile basi utamruzuku zaidi, na asipokila mwache.” Mtu yule hakukila mpaka akafa.”

76- Ibn Bashshaar amesema:

“Nilisoma kwenye kitabu kimoja cha kale: “Ee mwanaadamu! Usichelei kukosa riziki maadamu hazina Zangu zimejaa na hatu haziishi. Ee mwanaadamu! Kama jinsi sikuulizi juu ya matendo ya kesho basi na wewe usiniulize juu ya riziki ya kesho.”

77- ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Hakuna mtu yeyote isipokuwa atakuja kuikanyaga athari yake, kula riziki yake, kufikisha muda wake wa kuishi na kufa kifo chake. Lau mtu ataikimbia rikizi yake basi itamuwahi kama jinsi mauti yanavyomuwahi wakati anapoyakimbia.”

[1] at-Tirmidhiy (2406) na Ahmad (2/310). Swahiyh kupitia zingine kwa mujibu wa Ahmad Shaakir. Tazama “as-Swahiyhah” (930) ya al-Albaaniy.

 

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 51-57
  • Imechapishwa: 18/03/2017