Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

4- Yule mwenye kudai kujua kitu katika elimu ya ghaibu.

MAELEZO

Yule mwenye kudai… – Hapa wanaingia wachawi, wanajimu, makuhani, wapigaramli na kila mwenye kudai kuwa anajua ghaibu na anawaambia watu kwamba watapata kitu fulani na fulani, watapata furaha, watapata kitu katika uchovu au kwamba jambo fulani limekutana au halikukutana na ndoa. Watu hawa wanadai kujua mambo yaliyofichikana, mambo ambayo hakuna ayajuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema (Ta´ala):

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ

“Sema: “Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye yaliyofichikana isipokuwa Allaah.”[1]

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ فَإِنَّهُ يَسْلُكُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ رَصَدًا

”Mjuzi wa mambo yaliyofichikana na wala hamdhihirishii yeyote ghaibu Yake; isipokuwa yule aliyemridhia ambaye ni Mtume, basi hakika Yeye anamwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.”[2]

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ

 “Kwake zipo funguo za mambo yaliyofichikana; hakuna azijuaye isipokuwa Yeye tu. Anajua yale yote yaliyomo nchikavu na baharini; na halianguki jani lolote isipokuwa hulijua, na wala punje katika viza vya ardhi na wala kilichorutubika na wala kikavu isipokuwa kimo ndani ya Kitabu kinachobainisha.”[3]

Hapa kuna ufupizi. Hakuna ajuaye mambo yaliyofichikana isipokuwa Allaah au ambaye Allaah amemfunulia kitu katika mambo yaliyofichikana katika Mitume Yake kwa ajili ya manufaa ya watu au miujiza kwa Mtume. Lakini hakuijua ghaibu yeye kama yeye bali ameijua ghaibu baada ya kufunzwa na Allaah. Hakuna anayejua ghaibu isipokuwa Allaah. Yule mwenye kudai ghaibu basi hakika anakuwa amemshirikisha Allaah katika mambo ambayo amejisifu kuwa nayo Yeye pekee. Hivyo anakuwa ni mshirikina, Twaaghuut na kafiri. Hii ni aina moja wapo kubwa ya kumritadisha mtu nje ya Uislamu.

[1] 27:65

[2] 72:26-27

[3] 06:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 300-302
  • Imechapishwa: 24/02/2021