150. Ni lazima kwa mtu kujifunza dini na kuitendea kazi

Kupuuza – Maana yake ni kule kukikengeuka kitu pamoja na kutokuwa na shauku nacho.

Hajifunzi nacho – Mtu hajifunzi dini yake hali ya kuwa na shauku nayo. Huyu anakufuru kwa sababu haitakidi dini na wala haijali. Akipuuza kujifunza nayo anakufuru kwa kuwa hii ni dalili ya kuwa haitaki dini. Ikiwa haitaki dini hivyo anakufuru kwa sababu lau angelikuwa na hamu nayo basi angelijifunza nayo. Miongoni mwa watu hawa wanaingia wale ambao hii leo wanalingania kuondosha silebasi za dini kutoka katika ile mifumo ya masomo kwa sababu wanadai eti zinasababisha ugumu, upetukaji, ususuwavu na ugaidi.

Kadhalika yule mwenye kujifunza lakini hata hivyo haifanyii kazi, huyu pia anakufuru na kuritadi kutoka katika dini ya Uislamu. Ikiwa haswali, hafungi, hatoi zakaah, hahiji, hatekelezi mambo ya wajibu na kujiepusha na mambo ya haramu, yeye anajifunza tu pasi na kuyatendea kazi kwa kutokuwa na hamu ya matendo, huyu anakufuru. Hapa kuna Radd kwa Murji-ah ambao wanasema kuwa matendo sio ya lazima. Wanaona kuwa inatosha kuamini moyoni na kusadikisha moyoni hata kama mtu hakufanya matendo. Shaykh hapa amesema:

“Akiacha kufanya matendo.”

Akiyakataa matendo pamoja na kuwa ana uwezo juu yake, kwa mfano akakataa kuswali, amekataa kutoa zakaah, amekataa kufunga Ramadhaan, amekataa kuhiji Hajj ya faradhi, amekataa kujiepusha na mambo ya haramu na kutekeleza mambo ya wajibu, huyu anakufuru kwa sababu hakuifanyia kazi dini. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَمَن يَكْفُرْ بِالْإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Yeyote atakayeikanusha imani; basi kwa hakika yameporomoka matendo yake naye huko Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (al-Maaidah 05:05)

Ni lazima yapatikane mambo yote mawili; kujifunza mambo ya dini ambayo mtu hawezi kuitekeleza dini yake isipokuwa kwa mambo hayo na jengine ni kuyatendea kazi. Ni lazima kuwepo elimu na matendo. Dini haisimami bila ya matendo na matendo hayasimami isipokuwa kwa elimu. Ni mambo mawili yanayokwenda sambamba. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ

“Amemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili aidhihirishe juu ya dini zote.” (at-Tawbah 09:33)

Uongofu ni elimu yenye manufaa. Dini ya haki ni matendo mema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumilizwa kwa mambo mawili. Hakutumwa kwa elimu pekee na wala hakutumilizwa kwa matendo pekee, isipokuwa ametumilizwa kwa mambo yote mawili; ni mambo mawili yanayoenda sambamba.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 190-191
  • Imechapishwa: 13/03/2019