[1] Haikuwekwa Shari´ah isipokuwa msikitini tu. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ

“Na wala msichanganyike nao hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa I’tikaaf  misikitini.”[1]

´Aaishah amesema:

“Sunnah kwa yule mwenye kufanya I´tikaaf ni asitoke isipokuwa kwa haja inayomlazimu. Asimtembelee mgonjwa, asimguse mwanamke wake na wala asimwingilie. Akae I´tikaaf katika msikiti unaoswaliwa mkusanyiko. Sunnah pia kwa yule anayefanya I´tikaaf afunge.”[2]

[2] Inatakiwa kufanywa katika msikiti unaoswaliwa swalah ya ijumaa ili mtu asilazimike kutoka msikitini kwa ajili ya kuswali swalah ya ijumaa, kwa sababu kutoka kwa ajili ya kuiendea ni wajibu kwake. ´Aaishah amesema katika Hadiyth iliyotangulia:

“Hakuna I´tikaaf isipokuwa tu katika msikiti unaoswaliwa mkusanyiko.”

Baadaye nikaja kupata Hadiyth Swahiyh na inayosema wazi na kukhusisha “misikiti” iliyotajwa katika Aayah kwa ile misikiti mitatu; msikiti Mtakatifu, msikiti wa Mtume na msikiti wa al-Aqswaa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna I´tikaaf isipokuwa katika ile misikiti mitatu.”[3]

Salaf niliowakuta na maoni haya ni Hudhayfah bin al-Yamaan, Sa´iyd bin al-Musayyib na ´Atwaa´ isipokuwa yeye hakutaja msikiti wa al-Aqswaa. Kuna wengine wamesema ni sawa kwenye misikiti yote ambayo mtu anaswali swalah ya mkusanyiko. Baadhi ya wengine wakaenda kinyume na wakasema ni sawa vilevile hata katika msikiti wa nyumbani kwake. Hapana shaka ya kwamba lililo sahihi zaidi katika suala hili ni kutenda kazi kwa mujibu wa Hadiyth – na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye anajua zaidi.

[3] Lililo Sunnah kwa yule anayefanya I´tikaaf afunge, kama ilivyokwishatangulia katika Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa)[4]

[1] 02:187

[2] Ameipokea al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh na Abu Daawuud kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Upokezi hapa unaofuata utokamanao kwa ´Aaishah umepokelewa na yeye pia. Imetajwa katika “Swahiyh Abiy Daawuud” (2135) na “al-Irwaa´” (966).

[3] Ameipokea at-Twahaawiy, al-Ismaa´iyliy na al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh kutoka kwa Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ´anh). Imetajwa katika “as-Swahiyhah” (2786) pamoja na mapokezi yanayoafikiana nayo juu na yote ni Swahiyh.

[4] Ameipokea al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh na Abu Daawuud kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Imaam Ibn-ul-Qayyim amesema katika “Zaad-ul-Ma´aad”: “Haikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa alifanya I´tikaaf pasi na kufunga. Bali ´Aaishah amesema: “Hakuna I´tikaaf pasi na swawm.” Kadhalika Hakutaja (Subhaanah) I´tikaaf isipokuwa tu pamoja na swawm kama ambavyo vilevile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufanya hivo isipokuwa pamoja na swawm. Maoni yaliyo na nguvu katika dalili ni yale waliyomo Salaf, nayo ni kwamba kufunga ni sharti katika I´tikaaf na haya ndio maoni ambayo Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah alikuwa anaonelea kuwa na nguvu zaidi.” Kujengea juu ya hili haikuwekwa katika Shari´ah kwa yule aliyeenda msikitini kwa ajili ya kuswali au kitu kingine akanuia I´tikaaf kwa muda aliyoko huko. Haya ndio yaliyosemwa wazi na Shaykh-ul-Islaam katika “al-Ikhtiyaaraat”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 35-37
  • Imechapishwa: 07/05/2019