16. Ni yepi yanayojuzu wakati wa I´tikaaf?

[1] Inajuzu kwake kutoka kwa ajili ya kutekeleza dharura fulani au kutoa kichwa chake nje ya msikiti ili kioshwe na kichanuliwe. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akinitolea kichwa chake wakati anafanya I´tikaaf msikitini na mimi niko chumbani mwangu. Nikamtana [na katika upokezi mwingine: nikamuosha nikiwa katika hedhi yangu na hakuna kilichokuwa kikitutenganisha mimi na yeye isipokuwa tu kizingiti cha mlango] na pindi alipokuwa anafanya I´tikaaf alikuwa haingii nyumbani isipokuwa kwa sababu ya dharura fulani.”[1]

[2] Inajuzu kwa mwenye kufanya I´tikaaf na mwengineo kutawadha msikitini. Mwanamume aliyekuwa anamfanyia kazi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawadha msikitini wudhuu´ khafifu.”[2]

[3] Vilevile inafaa kwake kusimamisha hema dogo nyuma ya msikiti akawa anafanya I´tikaaf ndani yake. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwa amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimsimamishia Khibaa´[3] pindi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapofanya I´tikaaf[4].

Vilevile kuna wakati alifanya I´tikaaf kwenye kuba dogo ambayo mlango wake ulikuwa umefanywa kwa mkeka.

[1] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim, Ibn Abiy Shaybah na Ahmad na nyongeza ya kwanza ni ya kwao wawili. Imetajwa katika “Swahiyh Abiy Daawuud” (2131-2132).

[2] Ameipokea al-Bayhaqiy kwa mlolongo wa wapokezi mzuri na Ahmad (05/364) kwa ufupi kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[3] Khibaa´ ni kanyumba ka kiarabu kanakotokamana na manyoya au pamba, lakini sio nywele, na kamesimamishwa na nguzo mbili au tatu. (an-Nihaayah)

[4] Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa ´Aaishah. Kitendo ni cha al-Bukhaariy na amri ni ya Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 37-39
  • Imechapishwa: 07/05/2019