15. Du´aa katika Swalah na baada ya Tashahhud


82- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mmoja wenu atapomaliza Tashahhud ya mwisho aombe kinga kwa Allaah kutokana na mambo mane; adhabu ya Jahannam, adhabu ya kaburi, fitina ya uhai na ya kufa na shari ya al-Masiyh ad-Dajjaal.”

83- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba katika Swalah:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَةِ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْمَأْثَمِ وَالْمَغْرَمِ. قَالَتْ فَقَالَ لَهُ قَائِلٌ مَا أَكْثَرَ مَا تَسْتَعِيذُ مِنَ الْمَغْرَمِ يَا رَسُولَ اللَّهِ. فَقَالَ:إِنَّ الرَّجُلَ إِذَا غَرِمَ حَدَّثَ فَكَذَبَ وَوَعَدَ فَأَخْلَفَ

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba unihifadhi na adhabu za kaburi. Nakuomba unihifadhi na fitina ya al-Masiyh ad-Dajjaal. Nakuomba unihifadhi na fitina ya uhai na ya kufa. Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba unihifadhi na madhambi na madeni.” Mtu mmoja akamwambia: ”Ni wingi ulioje unaomba kinga kutokana na madeni.” Akasema: ”Wakati mtu anakuwa na deni husema uongo pale anapozungumza na huvunja ahadi pale anapoahidi.”

84- ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anhu) alisema kumwambia Mtume wa Allaah:

اللهم إني ظلمت نفسي ظلما كثيرا ولا يغفر الذنوب إلا أنت فاغفر لي مغفرة من عندك وارحمني إنك أنت الغفور الرحيم

”Ee Allaah! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu, dhulma iliokuwa kubwa. Hasamehi madhambi isipokuwa Wewe. Nisamehe msamaha kutoka Kwako na unirahamu. Wewe ni mwingi wa Kusamehe, mwingi wa Kurahamu.”

85- Katika ya mwisho ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema kati ya Tashahhud na Tasliym:

اللَّهُمَّ اغْفِرْ لي ما قدمت وما أَخرت وَمَا أَسْرَرْتُ وَمَا أَعْلَنْتُ و ما أسْرَفْتُ وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي أَنْتَ الْمُقَدِّم وأَنْتَ الْمُؤخِّر لاَ إِله إِلاَّ أَنْتَ

“Ee Allaah! Nisamehe dhambi nilizozitanguliza na nilizozichelewesha, nilizozificha na nilizozionesha, nilizozifanya kisiri na nilizozifanya kwa dhahiri, na nilizovuka mipaka na ambayo Wewe unazijua zaidi kuliko mimi. Wewe ndiye Mwenye kutanguliza na Wewe ndiye Mwenye kuchelewesha. Hapana mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe.”

86- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia mtu mmoja:

”Unasema nini katika Swalah yako?” Akasema: ”Ninasoma Tashahhud na ninasema:

اللَّهُمَّ إِني أَسْأَلُك الْجَنَّة وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ النَّارِ

”Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Pepo na najikinga kwako kutokana na Moto. Mimi siwezi kusema yale ambayo wewe na Mu´aadh mnayosema.” Hivyo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Na sisi tunasema kitu kinachofanana na hicho.”[1]

87- ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anhu) alisimama na kuswali Swalah fupi. Baadhi ya watu wakamwambia kwamba ameswali Swalah fupi. Akasema: ”Kuna nini kwa hicho? Pale nilikuwa naomba Du´aa ambayo nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiiomba.” Wakati aliposimama mtu mmoja akamfuata na kumuuliza Du´aa hiyo. Akasema:

اللَّهُمَّ بِعِلْمِكَ الْغَيْبَ وَقُدْرَتِكَ على الْخَلْقِ أَحْيِني ما عَلِمْتَ الْحَيَاةَ خَيْراً لِي وَتَوفَّني إِذَا عَلِمْتَ الْوَفَاةَ خَيْراً لِي اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ خَشْيَتَكَ في الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ وَأَسْأَلُكَ كَلِمَةَ الْحَقِّ في الرِّضَا وَ الْغَضبِ وَأَسْأَلُكَ الْقَصدَ في الْفَقْرِ والْغِنى وَأَسْأَلُكَ نَعِيماً لاَ يَنْفَدُ وَأَسْأَلُكَ قُرَّةَ عَيْنٍ لاَ تَنْقَطع وَأَسْأَلُكَ الرِّضَا بَعْدَ الْقَضَاءِ وَأَسْأَلُكَ بَرْدَ الْعَيْشِ بعد الْمَوتِ وَأَسْأَلكَ لَذَّةَ النَّظرِ إِلى وَجْهِكَ والشَّوْقَ إِلى لِقَائِكَ في غيرِ ضَرَّاءَ مُضِرَّةٍ وَلاَ فِتْنَةٍ مُضِلَّةٍ اللَّهُمَّ زَيِّنَّا بِزِينةِ الإِيْمانِ وَاجْعَلْنَا هُدَاةً مُهْتَدِينَ

“Ee Allaah! Ninakuomba kupitia Elimu Yako ya mambo yaliyofichikana na uwezo wa uumbaji Wako. Niweke hai mrefu endapo uhai ni bora kwangu. Nifishe endapo kufa ni bora kwangu. Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba kuwa na khofu Kwako katika siri na dhahiri. Ninakuomba kuzungumza neno la haki katika hali ya furaha na katika hali ya khasira. Ninakuomba uwastani katika utajiri na umaskini. Ninakuomba neema isiyokwisha. Ninakuomba furaha isiyokatika. Ninakuomba kuridhia baada ya kuwa umeshapanga (makadirio). Ninakuomba maisha mazuri baada ya mauti. Ninakuomba ladha ya kutazama Uso Wako na shauku ya kukutana na Wewe pasina madhara yanayodhuru wala fitina yenye kupoteza. Ee Allaah! Tupambe kwa kipambo cha imani na utufanye tuwe wenye kuongoka waongofu.”

88- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa akimaliza Swalah anaomba Allaah msamaha mara tatu na kusema:

اللَّهُمَّ أَنْتَ السَّلاَمُ وَمِنْك السَّلاَمُ تَبَارَكْتَ يَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرام

“Ee Allaah! Wewe ndiye Salaam na Kwako ndiko kunatoka Salaam. Umetukuka, Ewe Mwenye Utukufu na Ukarimu!”

89- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa akimaliza Swalah anasema:

لا إِلهَ إِلاَّ الله وَحْدَهُ لاَ شَريكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قَدِيرٌ اللَّهُمَّ لاَ مَانِعَ لما أَعْطَيْتَ وَلاَ مُعْطِي لِمَا مَنَعْتَ وَلاَ يَنْفَعُ ذَا الْجَدِّ مِنْكَ الجَدُّ

“Hakuna mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, Mmoja asiyekuwa na mshirika. Niwake Ufalme na himdi na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza. Ee Allaah! Hakuna awezae kukizuia Ulichokitoa na wala kutoa ulichokizuia. Tajiri hanufaiki na utajiri wake mbele Yako.”

90- ´Abdullaah bin az-Zubayr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba alikuwa akisema baada ya kila Swalah:

لا إِلهَ إِلا الله وَحْدَهُ لا شريكَ لَهُ لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ على كلِّ شَيءٍ قَدِيرٌ لاَ حَوْلَ وَلاَ قُوَّةَ إِلاَّ باللهِ لاَ إِلهَ إِلاَّ الله وَلاَ نَعْبُدُ إِلاَّ إِيَّاهُ لَهُ النِّعْمَةُ وَلَهُ الْفَضْلُ وَلَهُ الثَّنَاءُ الْحَسَنُ لا إِله إِلاَّ الله مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ

“Hakuna mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, Mmoja asiyekuwa na mshirika. Niwake Ufalme na himdi na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza. Hapana uwezo wala nguvu isipokuwa vyote vinatokana na Allaah. Hakuna mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, na wala hatumuabudu yeyote isipokuwa Yeye. Ni Zake neema na fadhila. Nizake sifa nzuri zote. Hakuna mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, hali ya kumtakasia dini, hata kama wanachukia makafiri.”

Ibn-uz-Zubayr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisoma haya baada ya kila Swalah.”

91- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) ameeleza kwamba Muhaajiruun mafukara walimjia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: ”Matajiri wameenda kwa daraja za juu na neema zenye kudumu; wanaswali kama tunavyoswali, wanafunga kama tunavyofunga na wana pesa za kutosha wanazojitolea katika Hajj, ´Umrah, Jihaad na Swadaqah.” Akasema: ”Nisiwafunze kitu ambacho mtawawahi wale waliowatangulia, mtawatangulia walio baada yenu na hakutokuwepo yeyote ambaye atakuwa bora kuliko nyinyi isipokuwa yule atayefanya mfano wa mliyoyafanya?” Wakasema: Ndio, ewe Mtume wa Allaah.” Akasema: ”Semeni ”Subhaan Allaah”, ”al-Hamdu lillaah” na ”Allaahu Akbar” baada ya kila Swalah mara thalathini na tatu.

Abu Swaalih, Taabiy´ katika Hadiyth, amesema:

”Ina maana kusema ”Subhaan Allaah”, ”al-Hamdu lillaah” na ”Allaahu Akbar” kila moja mara thalathini na tatu.”

92- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Anayesema baada ya kila Swalah ”Subhaan Allaah” mara thalathini na tatu, ”al-Hamdu lillaah” mara thalathini na tatu na ”Allaahu Akbar” mara thalathini na tatu na akakamilisha mia kwa kusema:

لاَ إِله إِلاَّ الله وَحده لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلكُ وَلَهُ الْحمدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَدِيرٌ

“Hakuna mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, Mmoja asiyekuwa na mshirika. Niwake Ufalme na himdi na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.”

anasamehewa madhambi yake hata kama yatakuwa mfano wa povu la bahari.”

93- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kuna sifa mbili ambazo mja Muislamu hatozihifadhi isipokuwa ataingia Peponi. Ni nyepesi na wenye kuzitendea kazi ni wachache. Baada ya kila Swalah aseme ”Subhaan Allaah” mara kumi, ”al-Hamdu lillaah” mara kumi na ”Allaahu Akbar” mara kumi. Ni mara 150 kwenye ulimi na ni mara 1500 kwenye mizani. Kadhalika wakati wa kulala aseme ”Allaahu Akbar” mara thalathini na nne, ”al-Hamdu lillaah” mara thalathini na tatu na ”Subhaan Allaah” mara thalathini na tatu. Ni mara 100 kwenye ulimi na ni mara 1000 kwenye mizani.”

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akizihesabu kwa mkono wake[2]. Wakasema: ”Ewe Mtume wa Allaah! Vipi zitakuwa nyepesi ilihali iwe ni wachache wanaozitendea kazi?” Akasema: ”Huja – yaani Shaytwaan – kwa mmoja katika nyinyi na kumfanya akasinzia kabla ya kuwahi kuzisema na huja kwa mmoja katika nyinyi na kumkumbusha haja zake kabla ya kuwahi kuzisema.”

94- ´Uqbah bin ´Aamir amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameniamrisha kusoma Suurat ”al-Falaq” na ”an-Naas” baada ya kila Swalah.”

95- Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anhu) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimshika mkono na kusema: ”Ewe Mu´aadh! Mimi ninaapa kwa Allaah nakupenda. Hivyo basi, usiache kusema baada ya kila Swalah:

اللَّهُمَّ أَعِنِّي على ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ

”Ee Allaah! Nisaidie kuweza kukukumbuka, kukushukuru na kukuuabudu vizuri.”

[1] Bi maana Du´aa zetu pia zinahusu kuingia Peponi.

[2] Bi maana kwa mkono wake wa kulia. Kufanya Tasbiyh kwa mikono yote miwili ni jambo linaenda kinyume na Sunnah. Ajabu ni kuona baadhi ya watu wanakula kwa mikono yao ya kushoto na wanafanya Tasbiyh kwa yote miwili.

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 61-68
  • Imechapishwa: 21/03/2017