142. Miongoni mwa dalili kwamba Allaah atawafufua viumbe baada ya kufa III


Miongoni mwa dalili juu ya kufufuliwa ni kwamba endapo kusingelikuwa kufufuliwa basi kungepelekea kuumbwa kwa watu ni mchezo mtupu kwa njia ya kwamba wanaishi na miongoni mwao wako ambao ni watiifu, wachaji na wanamwamini Allaah na Mtume Wake na wengine ni makafiri, wakanamungu, mazanadiki, wajeuri na watenda maasi. Wote wanaishi kisha wanakufa pasi na muumini huyu kupata kitu katika malipo yake au kafiri, zandiki, mkanajimungu na mjeuri huyu kupata chochote katika malipo yake. Je, hivi kweli inamstahikia Allaah kuwaacha watu namna hii pasi na kuwalipa waumini kwa imani yao na watenda ihsaan kwa ihsaan yao na wahalifu na makafiri kwa uhalifu na ukafiri wao? Haya hayaendani na hekima ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hii amesema:

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

”Na ni vya Allaah pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili awalipe wale waliofanya maovu kwa yale waliyoyatenda na awalipe wale waliofanya mema kwa mema zaidi.”[1]

Haya hayawi isipokuwa siku ya Qiyaamah. Kadhalika katika maneno Yake (Subhaanah):

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ

“Je, wanadhania wale waliochuma mabaya Tuwafanye wawe sawa na wale walioamini na wakatenda mema na pia sawasawa uhai wao na kufa kwao? – uovu ulioje wanaouhukumu!”[2]

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

“Je, Tuwajaalie wale walioamini na wakatenda mema kama wenye kueneza ufisadi ardhini au tuwajaalie wachaji kama waovu?”[3]

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ

“Je, mlidhania kwamba Sisi Tulikuumbeni bila kusudio mcheze tu na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?”[4]

أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَن يُتْرَكَ سُدًى أَلَمْ يَكُ نُطْفَةً مِّن مَّنِيٍّ يُمْنَىٰ ثُمَّ كَانَ عَلَقَةً فَخَلَقَ فَسَوَّىٰ فَجَعَلَ مِنْهُ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالْأُنثَىٰ أَلَيْسَ ذَٰلِكَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ

”Je, anadhani mtu ataachwa bure? Hivi hakuwa tone kutokana na manii yanayomwagwa kwa nguvu, kisha akawa pande la damu, akamuumba na akamsawazisha, akamfanya namna mbili; mwanamme na mwanamke? Je, Huyo hakuwa ni muweza wa kuhuisha wafu?”[5]

Pia akamraddi kafiri aliyesema:

مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ

“Ni nani atakayehuisha mifupa hii ilihali imekwishaoza?”[6]

Ambapo akamjibu kwa kusema:

قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ الَّذِي جَعَلَ لَكُم مِّنَ الشَّجَرِ الْأَخْضَرِ نَارًا فَإِذَا أَنتُم مِّنْهُ تُوقِدُونَ

”Akasema: ”Ni nani atakayehuisha mifupa hii ilihali imekwishaoza na kusagika na kuwa kama vumbi?” Sema: ”Ataihuisha Ambaye aliianzisha mara ya kwanza Naye ni mjuzi wa kila kiumbe; ambaye amekujaalieni moto kutokana na miti ya kijani, kisha nyinyi mnauwasha.”[7]

Ambaye ameweza kuutoa moto wa kuchoma kutokana na miji ya kijani yenye umande – ambaye ameyaweza haya asiweze kumuhuisha maiti?

[1] 53:31

[2] 45:21-22

[3] 38:28

[4] 23:115

[5] 75:36-40

[6] 36:78

[7] 36:78-80

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 281-282
  • Imechapishwa: 17/02/2021