14. Ubainifu wa msingi wa nne katika Qur-aan

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Allaah (Ta´ala) amebainisha msingi huu mwanzoni wa Suurah “al-Baqarah” kuanzia katika maneno Yake:

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ

“Enyi wana wa israaiyl! Kumbukeni neema Yangu niliyokuneemesheni…” (02:40)

mpaka katika maneno Yake kabla ya kutaja Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ

“Enyi wana wa israaiyl! Kumbukeni neema Yangu niliyokuneemesheni na hakika Mimi Nimekufadhilisheni juu ya walimwengu.” (02:122)

Hilo linazidi zaidi kuwa wazi na yale yaliyosemwa waziwazi na Sunnah katika maneno haya mengi yaliyo wazi kwa mjinga aliye mpumbavu.

MAELEZO

Allaah (Ta´ala) amebainisha msingi huu mwanzoni wa Suurah “al-Baqarah”… Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika “al-Baqarah” ameteremsha Aayah nyingi kuhusu wana wa israaiyl ili kuwakumbusha neema za Allaah juu yao na akawaamrisha kumfuata Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye wanajua utume na ujumbe wake kupitia vitabu vyao na alibashiriwa na Mitume wao. Kuanzia katika maneno Yake (Ta´ala):

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَوْفُوا بِعَهْدِي أُوفِ بِعَهْدِكُمْ

“Enyi wana wa Israaiyl! Kumbukeni neema Yangu niliyokuneemesheni na timizeni ahadi Yangu nikutimizieni ahadi yenu.”

Akaimalizia kwa kusema:

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا تَنفَعُهَا شَفَاعَةٌ وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ

“Enyi wana wa israaiyl! Kumbukeni neema Yangu niliyokuneemesheni na hakika Mimi nimekufadhilisheni juu ya walimwengu. Na iogopeni siku ambayo nafsi haitoifaa nafsi nyingine kwa lolote, wala haitokubaliwa kutoka kwake kikomboleo wala hautamfaa uombezi wala hawatonusuriwa.” (02:122-123)

Kisha sasa ndio akatajwa Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

وَإِذِ ابْتَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ رَبُّهُ بِكَلِمَاتٍ

“Na pindi alipojaribiwa Ibraahiym na Mola Wake kwa maneno… ” (02:124)

Aayah zote hizi, zilizo kati ya Aayah ya kwanza mpaka ya mwisho, ni Aayah nyingi. Zote zimezungumzia juu ya wana wa Israaiyl, kuwakumbusha neema za Allaah, kutumwa Mitume, kuteremshwa vitabu na kwamba lililo la wajibu kwao ni kumwamini Mtume wa Allaah ambaye ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Wana wa israaiyl ni watoto wa Ya´quub. Israaiyl ni Ya´quub. Wana wa israaiyl ni katika kizazi chake. Ni makabila kumi na mbili. Kila mtoto katika watoto wake akawa na dhuriya. Kila dhuriya ikaitwa kabila kama yalivyo makabila ya waarabu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقَطَّعْنَاهُمُ اثْنَتَيْ عَشْرَةَ أَسْبَاطًا أُمَمًا

“Na Tukawagawanya makabila kumi na mbili.” (07:160)

Hilo linazidi zaidi kuwa wazi… – Kuna Hadiyth zimepokelewa ambazo zinakokoteza na kupendekeza kujifunza elimu na kubainisha ni elimu ipi yenye manufaa na ni elimu ipi isiyokuwa na manufaa makubwa. Mtu akirejea kitabu “Jaamiy´ Bayaan-il-´Ilm wa Fadhwlih” cha Ibn ´Abdil-Barr au wengineo atajua jambo hili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 18/05/2021