135. Kufaradhishwa kwa Shari´ah zengine na kwamba Uislamu utabaki hadi kisimame Qiyaamah


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili juu ya Hijrah kutoka katika Sunnah, ni kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hijrah haitosimama mpaka Tawbah isimamishwe. Na Tawbah haitosimamishwa mpaka jua lichomoze kutoka magharibi.”

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotulia al-Madiynah, alifaradhishiwa Shari´ah zingine za Kiislamu. Kwa mfano zakaah, swawm, hajj, adhaana, Jihaad, kuamrisha mema na kukataza maovu na Shari´ah zingine za Kiislamu. Aliyafanya haya kwa miaka kumi. Baada ya hapo akafa, lakini Dini yake imebaki.

Hii ndio Dini yake. Hakuna kheri yoyote isipokuwa amewaonesha nayo Ummah wake, na hakuna shari yoyote isipokuwa amewatahadharisha nayo. Kheri [kubwa] Aliyowaonesha nayo ni Tawhiyd na kila anachokipenda Allaah na kukiridhia. Na shari [kubwa] Aliyowatahadharisha nayo ni shirki na kila anachokichukia Allaah na kukikataa.

Allaah amemtuma kwa watu wote na Allaah akafaradhisha kwa viumbe wote – majini na watu – kumtii. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.””[1]

MAELEZO

Ni kama tulivyotangulia kutaja kwamba Shari´ah iliteremka hatua kwa hatua mpaka Shari´ah ikakamilika. Kabla ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Allaah akamteremshia:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[2]

Baada ya kuteremka Aayah hii kwa kipindi kifupi ndipo akafariki  Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na dini yake itabaki hadi kisimame Qiyaamah.

[1] 07:158

[2] 05:03

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 270-271
  • Imechapishwa: 11/02/2021