8- Eda ya talaka imefungamana na hedhi. Mume akimtaliki mke wake baada ya kufanya naye jimaa au baada ya kuwa faragha naye basi ni wajibu kwake kukaa eda kwa kupata hedhi mara tatu ikiwa kama anapata hedhi na hana ujauzito. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالْمُطَلَّقَاتُ يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ ثَلَاثَةَ قُرُوءٍ

“Na wanawake waliotalakiwa wabakie kungojea [wasiolewe] quruu´ [twahara au hedhi] tatu.” (02:228)

Ikiwa kama ana mimba atakaa eda mpaka pale atapojifungua. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ

“Na wenye mimba muda wao [wa eda] watakapozaa mimba zao.” (65:04)

Na ikiwa bado ni kijana sana au ni mzee au alifanya operesheni ukeni na mengineyo na si mwenye kupati hedhi, eda yake ni miezi mitatu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاللَّائِي يَئِسْنَ مِنَ الْمَحِيضِ مِن نِّسَائِكُمْ إِنِ ارْتَبْتُمْ فَعِدَّتُهُنَّ ثَلَاثَةُ أَشْهُرٍ وَاللَّائِي لَمْ يَحِضْنَ

“Na wale wanawake wanaokata tamaa [wanaokoma] hedhi miongoni mwa wanawake wenu, mkiwa na shaka [katika muda wao wa eda], basi eda yao ni miezi mitatu, na [hiyo pia ni eda ya] wale wanawake wasiopata hedhi.” (65:04)

Na ikiwa kawaida ni mwenye kupata hedhi lakini kwa sababu fulani hedhi yake ikakatika kwa sababu ya ugonjwa, kunyonyesha au sababu nyengineyo, ni mwenye kubaki katika eda mpaka pale hedhi yake itaporudi hata kama itakawia.

Na ikiwa sababu hiyo itaondoka katika maradhi au kunyonyesha na hedhi isirudi, basi atasubiri/kukaa eda mwaka mmoja tangu pale sababu ilipoondoka. Haya ndio maoni sahihi yenye kuafikiana na kanuni za Kishari´ah. Mwanamke ambaye sababu imeondoka na hedhi yake isiwe ni yenye kurudi ni kama mwanamke ambaye hedhi yake imesita bila ya sababu yenye kujulikana. Mwanamke kama huyu atasubiri mwaka mmoja kikamilifu; miezi tisa kwa ajili ya mimba kwa sababu ya usalama na miezi tatu kwa ajili ya eda.

Ama ikiwa talaka itatokea baada ya kufunga ndoa lakini kabla ya jimaa na kabla ya kuwa faragha, basi hana eda ya talaka. Haijalishi kitu sawa akiwa ni mwanamke mwenye kupata hedhi au mwengineo. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا

“Enyi mlioamini! Mnapofunga nikaah [kuwaoa] Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kuwagusa [jimai], basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu.” (33:49)
  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016