7- Ni haramu kwa mume kumtaliki mke wake wakati yuko na hedhi. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ

“Ee Nabii! Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda [twahara na si katika hedhi au katika twahara mliyowaingilia].” (65:01)

Bi maana pale wanawake wanapoenda katika eda inayojulikana. Hali kama hiyo inakuwa wakati mume anapomtaliki wakati yuko na mimba au katika twahara ambayo hakumwingilia. Hakwenda katika eda ikiwa ataachika wakati yuko na hedhi kwa sababu eda haianzi kuhesabika katika hedhi aliyoachika. Hali kadhalika si mwenye kwenda katika eda akiachika katika twahara aliyomwingilia kwa sababu anakuwa si mwenye kujua kama amepata ujauzito katika jimaa hiyo ili aweze kukaa eda ya mjamzito au hakupata ujauzito ili aweze kukaa eda ya mwenye hedhi. Pale ilipokuwa hakuna yakini ni eda aina ipi itayotumika, ndipo ikawa ni haramu kumtaliki mpaka mambo yabainike.

Kutokana na Aayah iliyotangulia ni jambo la haramu kumtaliki mwanamke mwenye hedhi. Vilevile imethibiti katika al-Bukhaariy, Muslim na wengine kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye alimtaliki mke wake wakati yuko na hedhi. Wakati ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alipomweleza hilo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakasirika na kusema:

“Muamrishe amrudishe na abaki naye mpaka atwaharike. Kisha apate hedhi na kutwaharika tena. Halafu akitaka abaki naye au amtaliki kabla ya kumwingilia. Hiyo ndio eda ambayo Allaah ameamrisha kuwataliki wanawake kwayo.”[1]

Mwanaume akimtaliki mke wake ilihali yuko na hedhi ni mwenye kupata dhambi. Ni juu yake kutubu kwa Allaah (Ta´ala) na kumrejesha mke wake ili amtaliki talaka ya Kishari´ah na yenye kuafikiana na maamrisho ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya hapo amwache mpaka atwaharike na hedhi ambapo alimtaliki ndani yake halafu apate hedhi tena na kutwaharika. Baada ya hapo akitaka atabaki naye au atamtaliki kabla ya kumwingilia.

[1] al-Bukhaariy (5251) na Muslim (1471).