12. Da´wah inayowaridhisha watu wote


Nilikutana na baadhi ya vijana wa al-Ikhwaan al-Muslimuun. Niliona jinsi wanavohifadhi swalah na kuonesha hamasa za kijumla juu ya Uislamu. Nikaanza kuwaeleza mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kipingamizi chao ilikuwa kiongozi wa jumla (Hasan al-Bannaa) aliwatahadharisha juu ya mambo kama hayo kwa kuwa yanawafarikanisha waislamu. Kubwa walilokuwa wakilenga ni kusimamisha adhabu za Kishari´ah (Huduud) na serikali ya Kiislamu yenye kutekeleza Shari´ah kabla au baadae hata kama itakuwa kwa njia ya uasi na kupambana na watawala ambao walikuwa wakionelea kuwa ni makafiri, madhalimu au mafusaki kutokana na uelewa wao wa Aayah tukufu:

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.”[1]

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio madhalimu.” [2]

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio mafasiki.”[3]

Allaah akataka niende na baadhi ya vijana wa al-Ikhwaan kumtembelea kiongozi wa jumla Hasan al-Bannaa kwenye kituo kikuu cha kundi maeneo Hilmiyyah. Darsa ikaangukia siku ya Jumapili wakati walipokuwa na darsa yao ya wiki. Nikaisikiliza ikiwa ni kati ya fujo za Takbiyr na Tahmiyd. Kama ilivo mfumo wao. Nikaona namna anavyozungumza kwa hamasa na kuingilia maudhui mbali mbali. Akizifungamanisha na Aayah za Qur-aan na Hadiyth. Akatuhubiria na kutusomea kwa muda mrefu. Lakini hata hivyo katu hakuzungumzia ´Aqiydah sahihi ya Kiislamu. Hakuwakumbusha umati huu wa watu juu ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swiffaat. Aliashiria tu japo kwa mbali kabisa Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na kutosheka na hilo. Mazungumzo yake juu ya Uislamu yalikuwa ni ya kijumla. Hivyo alikuwa ni mwenye kuweza kumridhisha kila Suufiy, Ash´ariy, Mu´taziliy, Shi´iy, Khaarijiy… Lakini muislamu mwenye uelewa wa ´Aqiydah ya kundi lililookoka (Firqat-un-Naajiyah) anajua kuwa haina maana yoyote.

Allaah (Ta´ala) ametujaalia upambanuzi na wanachuoni masomo haya siku zote ndio ilikuwa shughuli yao kubwa. Khutbah zao na mihadhara yao ilikuwa inahusiana na mada zote, lakini hawazungumzi Khutbah yoyote wala mawaidha yoyote isipokuwa wanaingia katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah, Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swiffaat na wakikemea kutawassul kwa maiti, kujifungamanisha na makaburi na kuwafuata kichwa mchunga mababu na Mashaykh pasina dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Walikuwa wakibainisha madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah yenye kwenda kinyume na mapote yaliyopinda kama Ash´ariyyah, Mu´tazilah na mengineyo. Hili al-Ikhwaan al-Muslimuun hawataki kulizungumzia kwa sababu wanadai kuwa wanapupia kuukusanya Ummah juu ya ´Aqiydah mbali mbali.

Kadiri na jinsi tulivyoona hamasa za Hasan al-Bannaa na wafuasi wake kiasi hicho hicho nilikuwa na wasiwasi juu ya umati mkubwa wa watu kutoshikamana na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika misingi. Nilikuwa nikisoma jarida la “al-Ikhwaan al-Muslimuun” na magazeti yao pasina kuona chenye kunipa matumaini ya harakati za kundi hili[4].

[1] 05:44

[2] 05:45

[3] 05:47

[4] al-Ikhwaan al-Muslimuun, uk. 53, ya ´Aliy al-Waswifiy.

Mwandishi: Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab al-Bannaa
Marejeo: Lamahaat ´an Da´wat-il-Ikhwaan al-Muslimiyn, uk. 35-36
Mkusanyaji: Muhammad bin ´Iwadhw bin ´Abdil-Ghaniy