113. Dalili ya Ihsaan kutoka katika Sunnah III


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Uislamu ni kushuhudia kuwa hapana mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji ukiweza.” Akasema: “Umesema kweli.” Tukashangazwa kwa kumuuliza kwake Mtume na kumsadikisha.

MAELEZO

Akasema: “Uislamu ni kuhushudia kuwa… – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtajia nguzo za Uislamu ambazo ni lazima na ambazo zikihakikika na kupatikana basi Uislamu umehakikika. Yenye kuzidi juu yake katika mambo mengine ni yenye kukamilisha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafupika katika kubainisha nguzo za Uislamu. Kwa sababu jinsi ambavo jibu linakuwa fupi ndivo linavokuwa jepesi kwa mwanafunzi na msikilizaji na inakuwa rahisi kwake kulihifadhi na kulielewa. Sambamba na hilo jibu likiwa gumu kwa wahudhuriaji na pengine hata wengi wao hawatolifahamu. Hii ni dalili inayoonyesha kuwa muulizwaji anapaswa kulenga ufupizaji kiasi cha inavowezekana na akifanye kitu cha kilazima. Vinginevyo Uislamu ni mpana zaidi ya hivo. Hizi ni nguzo zake ambazo umesimama juu yake.

Akasema: “Umesema kweli.” – Hii ni ajabu ya pili.

Wakashangazwa kwa kumuuliza… – Ni dalili inayoonyesha kuwa anajua na kwamba haulizi kwa sababu hajui. Anauliza hali ya kuwa anajua. Dalili ya hilo ni kwa sababu alisema:

“Umesema kweli.”

Ni dalili inayoonyesha kuwa anajua. Ni kwa nini anauliza?

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 232-233
  • Imechapishwa: 01/02/2021