Ni lazima kwa kila muislamu kuyategemeza mambo yake kwa Allaah (´Azza wa Jall), hali ya kuwa ni mwenye kutarajia fadhilah na neema Zake na mwenye kumtegemea Yeye. Kwani mambo yote yako mikononi mwa Allaah. Waislamu wote wanapaswa kuhakikisha ni wenye kukabiliana na misiba yote inayowafika kwa kuwa na subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah. Allaah amewaahidi wale wenye kusubiri ujira mkubwa:

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

“Hakika wale wenye kusubiri watalipwa kikamilifu ujira wao pasi na hesabu.”[1]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu tauni ambapo akajibu:

“Ni adhabu ambayo Allaah huiaigiza kwa Anayemtaka. Allaah akaifanya kuwa ni rehema kwa waumini. Hakuna mja yeyote ambaye kitatokea tauni ambapo akabaki katika mji wake hali ya kuwa ni mwenye kusubiri na akatambua kuwa hakuna kitachomfika isipokuwa kile ambacho Allaah alimwandikia, isipokuwa atakuwa na mfano ujira wa shahidi.”[2]

Namuomba Allaah atuwafikishe sote katika yale anayoyapenda na kuyaridhia katika matendo mema – kwani hakika Yeye ndiye mwenye kusema kauli ya haki na ndiye mwenye kuongoa njia. Himdi zote njema ni za Allaah pekee. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] 39:10

[2] al-Bukhaariy.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Ashru Waswaayaa lil-Wiqaayah min-al-Wabaa’, uk. 13-15
  • Imechapishwa: 05/04/2020