Ndugu! Ziumeni kwa magego Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), fuateni njia ya Salaf kisha mtazame kama hilo litakudhuruni na kitu. Pengine wale ambao ni wenye kupupia katika Bid´ah ni wenye kuzembea kwa mambo ambayo yamethibiti katika Shari´ah na Sunnah. Wanapomalizana na Bid´ah zao wanaenda kuzitumia vibaya Sunnah zilizothibiti. Hii ndio natija ya madhara ya Bid´ah. Bid´ah ina madhara makubwa kwenye mioyo na khatari ilio kubwa katika dini. Hakuna mtu wa Bid´ah yeyote mwenye kuzua katika dini ya Allaah isipokuwa hukosa kiwango hichohicho cha Sunnah au zaidi yake, kama walivyosema baadhi ya wanazuoni wa Salaf.

Pindi mtu anapohisi kuwa anafuata na hazui basi huhisi khofu kamili, unyenyekevu, udhalilifu na ´ibaadah kwa Mola wa walimwengu. Vivyo hivyo huhisi kuwa anamfuata kikamilifu kiongozi wa wachaji Allaah, bwana wa Mitume na Mtume wa Mola wa walimwengu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mimi nawanasihi ndugu zangu wote ambao kwa njia moja au nyingine wameona Bid´ah fulani kuwa ni nzuri – ni mamoja ikiwa inahusiana na dhati ya Allaah, majina na sifa au kumuadhimisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – kumcha Allaah na waachane na jambo hilo. Wafanye dini yao iwe imejengwa juu ya kufuata na sio kuzua, kumpwekesha Allaah peke yake na sio kumshirikisha na chochote, kufuata Sunnah na sio kuigiliza Bid´ah. Wafanye yale anayoyapenda Mwingi wa huruma na sio yale yanayopendeza kwa Shaytwaan. Halafu wataona jinsi nyoyo zao zitavyokuwa na usalama, uhai, utulivu, raha na nuru kubwa.

Ninamuomba Allaah (Ta´ala) atufanye kuwa waongofu wenye kuongoza na viongozi wenye kutengeneza, kuiangaza mioyo yetu na imani na elimu na asifanye yale tuliyojifunza yakawa dhidi yetu. Ninamuomba Allaah atuongoze katika njia ya waja Wake waumini na atufanye kuwa miongoni mwa mawalii Wake wenye kumcha na kundi lililoshinda.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ibdaa´ fiy Kamaal-ish-Shar´ wa Khatwar-il-Ibtidaa´, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 23/10/2016