Ndugu! Ili kitendo kiwe ni chenye kuafikiana na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kinahitaji kiwe ni chenye kuafikiana na mambo sita ya Shari´ah:

1 – Sababu. Mtu akimuabudu Allaah kwa sababu ambayo haiafikiani na Shari´ah ni yenye kurudishwa. Kwa mfano baadhi ya watu wanakesha na kuswali usiku wa tarehe ishirini na saba Rajab kwa sababu wanaona kuwa ndio usiku ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipandishwa mbinguni. Swalah ya usiku ni ´ibaadah, lakini ikifanywa kwa sababu hii ni Bid´ah. Kwa sababu ´ibaadah hii imeambatanishwa na sababu ambayo haikubaliwi kwa mujibu wa Shari´ah. Nukta hii ni muhimu na inaweka wazi matendo mengi ambayo yanachukuliwa kuwa ni Sunnah na wakati ukweli wa mambo sio Sunnah.

2 – Aina. Aina ya ´ibaadah ni lazima iwe yenye kuafikiana na Shari´ah. Aina ya ´ibaadah ambayo haikuwekwa katika Shari´ah na Allaah haikubaliwi. Kwa mfano mtu akachimja farasi wakati wa ´Iyd-ul-Adhwhaa. Kitendo hichi sio sahihi kwa sababu kinaenda kinyume na aina ya kitendo kilichowekwa katika Shari´ah. Wanyama wanaotakiwa kuchinjwa katika ´Iyd-ul-Adhwhaa ni wanyama wa kufuga kama mfano wa ngamia, ng´ombe na kondoo.

3 – Kiwango. Lau mtu atataka kuongeza swalah ya faradhi ni Bid´ah isiyokubaliwa kwa sababu inaenda kinyume na kiwango kilichowekwa katika Shari´ah. Hali kadhalika kwa mfano mtu atataka kuswali Dhuhr Rak´ah tano. Swalah kama hii haisihi kwa makubaliano.

4 – Namna. Kwa mfano mtu akaanza kutawadha kwa kuosha miguu, kupangusa kichwa, kuosha mikono na mwishoni akamalizia kwa kuosha uso. Wudhuu´ wake ni batili kwa sababu unaenda kinyume na Shari´ah.

5 – Wakati. Kwa mfano mtu akachinja mnyama wake wa Udhhiyah mwanzoni mwa Dhul-Hijjah. Kichinjwa chake cha Udhhiyah hakikubaliki kwa sababu kinaenda kinyume na wakati wa Shari´ah.

Nimesikia kuwa kuna watu wanachinja kondoo katika Ramadhaan kwa ajili ya ´ibaadah. Kitendo hichi ni Bid´ah kwa sura kama hii. Kichinjwa kinachochinjw kwa ajili ya ´ibaadah ni kile kinachokuwa katika mnasaba wa ´Iyd-ul-Adhwhaa, hajj na ´Aqiyqah. Kuhusu kuchinja katika Ramadhaan kwa kutarajia ya kwamba kichinjwa kinakuwa na thawabu kama thawabu zinazopatikana katika ´Iyd-ul-Adhwhaa ni Bid´ah. Hata hivyo inajuzu kuchinja kwa ajili ya kula nyama.

6 – Maeneo. Kwa mfano mtu akafanya I´tikaaf pasipokuwa msikitini. I´tikaaf yake hii haisihi. I´tikaaf haifanywi isipokuwa misikitini. Vivyo hivyo endapo mwanamke atataka kufanya I´tikaaf mahali pa kuswali nyumbani; kitendo chake hichi si sahihi kwa sababu kinaenda kinyume na Shari´ah inapokuja katika maeneo. Mfano mwingine ni kama mtu anafanya Twawaaf nyuma ya msikiti kwa sababu ya msongamano uliopo kwenye Ka´bah. Kitendo chake si sahihi kwa sababu Twawaaf inafanywa kwenye Ka´bah. Allaah (Ta´ala) amesema kumwambia kipenzi Chake mwandani Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَطَهِّرْ بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ

“Na isafishe Nyumba Yangu kwa wafanyao Twawaaf.”[1]

´Ibaadah haiwezi kuwa kitendo chema isipokuwa ikiwa imetimiza masharti mawili:

1 – Ifanywe kwa ajili ya Allaah.

2 – Kiafikiane na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokamana na nukta sita tulizotaja.

Mimi nawaambia wale waliopewa mtihani wa Bid´ah na ambao huenda wakawa na nia nzuri: Naapa kwa Allaah ya kwamba hatujui njia yoyote ilio bora zaidi kushinda njia ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum).

[1] 22:26

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ibdaa´ fiy Kamaal-ish-Shar´ wa Khatwar-il-Ibtidaa´, uk. 1416
  • Imechapishwa: 23/10/2016