Vivyo hivyo wale wanaofanyia istihzai Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba eti ni mambo madogomadogo. Kwa mfano kufuga ndevu na kupunguza masharubu ni katika mambo madogomadogo na kwamba nyinyi mnajishughulisha na mambo madogomadogo. Vilevile wanasema kutumia Siwaak ni katika mambo madogomadogo na kwamba wanaume kutovaa nguo inayovuka kongo mbili za miguu ni katika mambo madogomadogo.  Wanasema watu waachwe wavae watakacho, wanawake kuvaa vibaya ni katika ukamilifu na kwamba Hijaab ni katika mambo madogomadogo. Kumebaki nini tena? Dini yote sasa imekuwa ni mambo madogomadogo. Bali wanasema kuwa shirki na kuyaabudu kuabudu ni katika mambo mepesi. Wanasema kuwa hivi ndivo wanavoamini na kwamba wako huru katika imani yao, kwamba watu wanatakiwa kuheshimu mtazamo wa wengine, kila mmoja ana mtazamo wake, kwamba wao ni Mujtahiduun, wasifanyiwe ukali na wala wasikaripiwe. Yote haya yanasemwa hivi leo. Hapana shaka kwamba huku ni kupingana na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ni kuponda Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ikiwa Qur-aan na Sunnah vimetuletea vitu vidogovidogo, kumebakia nini tena?

Wanasema hebu tuwe na umoja hata kama kati yetu kutakuwepo wenye kuabudu makaburi na Shiy´ah ili tukabiliane na makafiri. Tunawauliza ni nini maana ya ukafiri? Wanasema kwamba maana ya ukafiri ni kupinga kuwepo kwa Muumba. Hii ndio kufuru. Tunawauliza “Vipi shirki na kumuabudu mwingine asiyekuwa Allaah sio kufuru?” Bali ni katika ukafiri mkubwa kabisa. Ambaye anamtukana Allaah, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na anawatukana Maswahabah, huu ndio ukafiri mbaya kabisa. Yule ambaye anawatukana Maswahabah, anamponda mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na anamsakama kitu alichomtakasa nacho Allaah, huyu anamponda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumtuhukumu kwamba mke wake ni muovu na kuwa anayakubali maovu kwa mke wake. Tunamuomba Allaah afya. Anaona kwamba Allaah kamchagulia Mtume wake mke ambaye ni mbaya. Huku ni kumtukana Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba Allaah kamchagulia Mtume wake mke mbaya na Mtume kamridhia ilihali ni mbaya. Hii ni kufuru ya waziwazi isiyokuwa na mashaka yoyote.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 135-136
  • Imechapishwa: 24/12/2018