Mtu anaweza kupatwa na uchawi. Uchawi ni maradhi khatari. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwahi kurogwa na myahudi mmoja. Lakini dawa yake ilikuwa kwa kutumia mambo yanayoruhusu. Dawa yake ilikuwa kwa kutumia matabano ya Kishari´ah na du´aa zinazoruhusu.

“Allaah hakuteremsha maradhi yoyote isipokuwa kateremsha pia dawa yake. Kajua yule aliyeuijua na hakuijua yule ambaye hakuijua.”

Ama kutibu uchawi kwa kutumia uchawi, hii ni kufuru na kumshirikisha Allaah na kuiharibu ´Aqiydah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si katika sisi yule atayefanya ukuhani au akafanyiwa ukuhani, atakayetafuta au akaomba kubashiriwa mikosi ya ndege, akafanya uchawi au akaomba kufanyiwa uchawi.”

Haijuzu kuwaendea wachawi na waganga kwa hali yoyote ile. Kwa sababu mtu akiwaendea ina maana ameridhia matendo yao. Kazi yao ni kumkufuru Allaah:

وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ

“… lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu uchawi.” (02:102)

Kujifunza uchawi na kuufunza ni kufuru:

وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

“Na [hao Malaika wawili] hawamfundishi yeyote mpaka wamueleze: “Hakika sisi ni mtihani, hivyo basi usikufuru [kufanya uchawi].” (02:102)

Hii ni dalili inayofahamisha kwamba uchawi ni kufuru. Ni mamoja kule kujifunza na kuufunza. Hali kadhalika kujitibu nao. Haijuzu kwa mtu kwenda kwa wachawi ili kujitibu kwao kwa uchawi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanyiwa uchawi na uchawi ukamuathiri (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Yeye ni mtu wa kawaida anasibiwa na yanayoweza kuwasibu watu wengine katika maradhi, madonda n.k. Lakini hata hivyo alijitibu kwa kufanya matabano. Alimjia Jibriyl (´alayhis-Salaam) na akamfanyia Ruqyah kwa kumsomea Qur-aan, du´aa, al-Ikhlaasw, al-Falaq na an-Naas. Allaah akamponya. Hii ndio njia ya kujitibu uchawi. Uchawi unatibiwa kwa Qur-aan, du´aa zinazoruhusu na dawa. Haijuzu kwake kwenda kwa wachawi kutibiwa kwao. Vipi atatibu maradhi ya mwili kwa kujisababishia maradhi ya ki-´Aqiydah na ya moyo?

Ni lazima kwake kumtegemea Allaah na wala asikate tamaa kwa Rahmah ya Allaah. Ajue kuwa ponyo iko mikononi mwa Allaah na kwamba faraja iko karibu. Anatakiwa amjengee dhana nzuri Allaah na huku akifanya sababu zilizoruhusiwa. Allaah (Jalla wa ´Alaa) Yuko karibu na ni Mwenye kujibu. Asikate tamaa. Lakini ailinde ´Aqiydah yake zaidi kuliko anavoyalinda maisha yake na mwili wake. Kwa sababu ikiharibika ´Aqiydah yake ameangamia na kukhasirika duniani na Aakhirah. Aidha kapotea upotofu  wa wazi. Ni wajibu kuzinduka juu ya hilo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah al-Islaamiyyah as-Swahiyhah https://www.youtube.com/watch?v=KqoTCYds6Cs&t=13s
  • Imechapishwa: 07/02/2019