Miogngoni mwa sababu za kufanya familia kuwa na furaha ni jambo ambalo wengi wamelikosa majumbani mwao hii leo. Nalo si lingine ni nyumbani kusimamishwe kumtaja Allaah (´Azza wa Jall). Kwa masikitiko makubwa wakati huu wanafamilia wetu wengi wamekosa kumtaja Allaah majumbani. Kunakaribia kutosomwa Qur-aan kwenye manyumba yao na katika baadhi ya majumba mengine Allaah anakaribia kutotajwa kabisa. Nyumba nyingi zimekuwa na utajo wa mashaytwaan ambao ni zile nyimbo na muziki unaowekwa kwenye majumba, jambo ambalo limepelekea kukosekana furaha kwenye manyumba mengi.

Ndugu wapendwa! Kitendo cha kuhifadhi kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) kinafungua kifua na kufanya moyo kupata utulivu. Je, si ni Mola wetu (Subhanaahu wa Ta´ala) ndiye kasema:

أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ

“Tanabahi! Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia!”? 13:28

Je, hatuna yakini? Je, sisi si waumini?

أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ

“Tanabahi! Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia!” 13:28

Nyumbani akitajwa Allaah basi mioyo inapata utulivu. Kumdhukuru Allaah kuna taathira kubwa katika kufungua kifua na kuondosha dhiki na hamu. Kwa ajili hii ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa yule ambaye anamtaja Allaah na yule asiyemtaja Allaah ni kama mfano wa aliye hai na maiti.” al-Bukhaariy (6407).

Yule mwenye kumtaja Allaah yuhai na yule asiyemtaja Allaah ni maiti hata kama atapita mbele za watu. Ni maiti asiyekuwa na uhai katika maisha yake na wala hakuna roho katika nyumba yake kwa kuwa hamdhukuru Allaah (´Azza wa Jall). Fadhila za kumtaja Allaah ni kubwa. Kumtaja Allaah ni miongoni mwa sababu kubwa za kuleta furaha. Kwa nini, ee mja wa Allaah? Kwa kuwa pindi unapomtaja Allaah (´Azza wa Jall) basi Allaah anakuwa mwenye kukuhifadhi. Ukiwa ni mwenye kujua kuwa Allaah anakuhifadhi sunajua ni mwenye raha moyoni? Ukijua kuwa Allaah ni muhifadhi na mjuzi moyo wako si unahisi raha? Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa shaytwaan alimwambia:

“Utapoenda kitandani mwako basi soma Aayat-ul-Kursiy mpaka utapoikamilisha Aayah. Hakika hutoacha kuendelea kuwa na mlinzi kutoka kwa Allaah na wala shaytwaan hatokukaribia mpaka kupambazuke.” Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) akamweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayo ambapo akamwambia: “Amekwambia ukweli japo ni mwongo.” al-Bukhaariy (2311), an-Nasaa´iy (959) na Ibn Khuzaymah (04/2424).

Ni vipi moyo wa muislamu usihisi raha kwa hifadhi ya Allaah ilihali anasoma mwisho wa Suurah “al-Baqarah”? Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayesoma Aayah mbili kutoka mwishoni mwa Suurah “al-Baqarah” basi zitamtosheleza.” al-Bukhaariy (5008) na matamshi ni yake na Muslim (807).

Anachotaka kusema ni kwamba zitamtosheleza kiibada. Hakika ni ´ibaadah kubwa usiku. Vilevile zitamtosheleza na kila shari kwa fadhila za Allaah. Allaah (´Azza wa Jall) atamhifadhi kwa hayo.

Ni vipi moyo wa muislamu usistareheke ilihali asubuhi na jioni anasema mara tatu: “Atakayesema ´Kwa jina la Allaah ambaye kwa jina Lake hakidhuru kitu ardhini wala mbinguni Naye ni Mwenye kusikia Mjuzi` hatofikwa na janga la ghafla mpaka kupambazuke. Yule atakayeyasema mara tatu pindi kunapopambazuka hatofikwa na janga la ghafla mpaka kuingie jioni”? Ahmad (01/62, 66 na 72), Abu Daawuud (5088) na (5089) na matamshi ni yake, at-Tirmidhiy (3388), Ibn Maajah (3869) na ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy na ameisahihisha al-Albaaniy katika “al-Mishkaah” (2391).

Atakayeyasema asubuhi basi Allaah atamsalimisha kutokamana na balaa za ghafla mpaka kuingie jioni na yule atayeyasema pindi inapofika jioni basi Allaah atamsalimisha kutokamana na balaa za ghafla mpaka kupambazuke. Ni vipi moyo usistareheke kwa jambo hili? Ni vipi moyo wa muumini usihisi utulivu, starehe na furaha ilihali anasoma Suurah “al-Ikhlaasw”, “an-Naas” na al-Falaq” kila asubuhi na jioni mara tatu? Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Soma: “Sema: “Hakika Allaah ni Mmoja, an-Naas na al-Falaq” pindi kunaingia jioni na asubuhi mara tatu zitakutosheleza dhidi ya kila kitu.”” Abu Daawuud (5082), at-Tirmidhiy (3575) ambaye amesema: “Nzuri, Swahiyh na geni.” al-Albaaniy amesema: “Nzuri Swahiyh” katika “Swahiyh Targhiyb wat-Tarhiyb” (649).

Ni vipi furaha itakosa kuchanganyika na moyo wako na dhiki, huzuni na masononeko yaondoke moyoni mwako ilihali unasema “Allaah ndiye Mola wangu asiyekuwa na mshirika”? Je, neno hili ni gumu kulihifadhi? Allaah ndiye Mola wangu asiyekuwa na mshirika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayepatwa na dhiki, hamu, uchungu au tatizo akasema “Allaah ndiye Mola wangu asiyekuwa na mshirika” itamuondoka.”” at-Twabaraaniy (24/396).

Ni sababu kubwa iliyoje miongoni mwa sababu za kuleta furaha! Lakini hata hivyo tumeghafilika nayo.

Nyumba ambayo kunasomwa ndani yake Suurah “al-Baqarah” mashaytwaan wanakimbia[1]. Lakini ni nani anayesoma Suurah “al-Baqarah” nyumbani kwake hii leo? Ni watu wachache mno. Kwa ajili hiyo ndio maana mashaytwaan wamekaa katika majumba mengi. Mtu pindi atapoingia nyumbani kwake na kusema: “Kwa jina la Allaah” basi shaytwaan hukimbia kutoka nyumbani na kusema “Leo hamna makazi wala mlo.”[2] Watu wengi wanaingia majumbani mwao pasi na kumtaja Allaah. Bali tumepata khabari ya kwamba baadhi ya watu wanaingia majumbani mwao na huku wanaimba na kupiga makofi. Watu kama hawa wanaingia pamoja na shaytwaan bali shaytwaan anamtangulia kuingia nyumbani. Vipi nyumbani kwake kutakuwa na furaha?

[1] Hayo yamethibiti katika Hadiyth ya Muslim (780).

[2] Muslim (2018).

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Asbaab sa´aadat-il-Usrah, uk. 23-27
  • Imechapishwa: 08/10/2016