Miongoni mwa mambo yanayohusiana na msingi huu ili kuifanya familia kuwa na furaha ni kuwa uchaguzi wa mume na mke uwe umejengwa juu ya kutazama dini pasi na kupuuza yale anayohitajia mtu katika kustareheka na yule atayeshirikiana naye katika maisha yake. Haya ndio yaliyoelekezwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema:

“Mwanamke anaolewa kwa mambo mane; kwa mali yake, ukoo wake, uzuri wake na kwa dini yake. Mchague yule mwenye dini utafaulu.”

Amekhabarisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba yanayovutia kumuoa mwanamke ni:

1- Mali yake.

2- Uzuri wake.

3- Ukoo wake.

4- Dini yake.

Akabainisha ya kwamba yule ambaye amefaulu ni ambaye amemchagua mwanamke wa dini. Ni uzuri uliyoje wa maneno ya aliyesema:

Msichana [mzuri] si kwa mali wala uzuri wake

sivyo! Wala [si] kwa kujifakhari kwa wazazi

Lakini ni kwa kujilinda na kwa kutwaharika kwake

na wema wake kwa mume na kwa watoto

Vilevile kusimamia kazi za nyumba yake

na akujali katika raha na shida

Ni wapi anapatikana msichana wa sampuli hii?

chini makuba ya bluu.

Ni wasichana wanaotafutwa kwa maji ya dhahabu. Bali wanatafutwa kwa hazina ya dhahabu. Anasema mteuliwa mchaguliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Akikujieni yule ambaye mnaridhia dini na tabia yake, basi muozesheni. Msipofanya hivo, basi kutakuwa fitina na ufisadi mkubwa.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanya kumchagua mume kuwe kumejengwa juu ya kutazama dini na tabia na akaashiria kuwa jambo hilo ni kubwa mno linalozuia fitina na kufanya ardhi na majumba kuwa mazuri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Oeni wanawake wenye mahaba na wenye kuzaa. Hakika mimi nitajifakhari juu yenu nyumati zingine.”

Pamoja na maelekezo haya makubwa kwa vile mtu ni mwanadamu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupuuza yale anayohitajia mtu ili maisha yake yapate kuwa na utulivu. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) anasimulia ya kwamba alikuwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akajiwa na mwanaume mmoja ambaye akamkhabarisha kuwa amemchumbia mwanamke katika Answaar kwa lengo la kutaka kumuoa. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Je, umemtazama?” Akasema: “Hapana.” Akamwambia: “Nenda umtazame.”

Kwa nini alimwambia hivo?

Akasema: “Kwa kuwa machoni mwa Answaar kuna kitu.”

Mwanaume huyu alikuwa ni katika Muhaajiruun. Alikuwa amemchumbia mwanamke katika Answaar. Akaja kumweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amemposa. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza kama amekwishamtazama ambapo akamjibu kuwa bado. Ndipo akamwambia: “Nenda umtazame!”

Kwa nini alimwambia hivo?

Kwa kuwa yeye ni Muhaajiriy na machoni mwa Answaariy kuna kitu kidogo ambacho huenda kisimfurahishe yule Muhaajiriy. Tazama namna Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyomwelekeza atazame kile kitachompendeza kwa vile ni mwanadamu. Hakupuuza upande huu.

Kadhalika imepokelewa kwamba al-Mughiyrah bin Shu´bah alimchumbia mwanamke. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Nenda ukamtazame. Kuna uwezekano mkubwa uhusiano wenu ukabaki.”

Akaenda na kumtazama. Tazama namna Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyomwelekeza al-Mughiyrah kwenda kumtazama mwanamke anayetaka kumuoa. Baada ya hapo akaeleza hekima. Nayo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wakadumu wakiwa pamoja na maisha yao yadumu juu ya furaha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutosheka na kule mwanaume kujua kuwa yule anayeenda kumchumbia ana dini. Bali alizingatia ile haja ya kiutu ambayo ni mtu afurahike na yule atayekuwa naye katika maisha yake. Jambo hili ni miongoni mwa sababu kubwa familia kupata utulivu. Mwanaume akimuoa mwanamke ambaye anastareheka naye na wakati huo huo mwanamke huyo akawa na dini, basi huwa ni furaha kwa familia yake na kudumu kwa uhusiano wake wa kindoa.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Asbaab sa´aadat-il-Usrah, uk. 17-23
  • Imechapishwa: 08/10/2016