06. Imani na faradhi vilishushwa hatua kwa hatua

Kuhusu hoja katika Sunnah na mapokezi yaliyopokelewa kwa wingi, baadhi ya Hadiyth zinataja matendo manne, zengine tano, zengine tisa na nyenginezo zaidi ya hivo. Kuhusu matendo mane yanasimamisha msingi wa imani ´Abbaad bin ´Abbaad al-Mahlabiy ametuhadithia: Abu Jamrah ametuhadithia, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Mjumbe wa ´Abdul-Qays alifika kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Sisi ni kabila linalotoka Rabiy´ah. Kati yako na sisi wako makafiri wanaotoka Mudhwar. Hatuwezi kufika kwako isipokuwa katika miezi mitukufu. Tuamrishe kitu tunachoweza kufanya na kuwalingania watu wetu.” Akasema: “Nakuamrisheni mambo manne na nakukatazeni mambo manne: “Imani… “

Kisha akawafasiria na kusema:

“Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, zakaah na mtoe khumusi ya ngawira zenu. Nakukatazeni kibuyu, balasi, shina la mtende lenye kutobolewa katikati na pombe ya tende.”

Kuhusu matendo matano Ishaaq bin Sulaymaan ar-Raaziy ametuhadithia, kutoka kwa Handhwalah bin Abiy Sufyaan, kutoka kwa ´Ikrimah bin Khaalid, kutoka kwa Ibn ´Umar aliyesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Uislamu umejengwa juu ya matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kuhiji nyumba ya Allaah na kufunga Ramadhaan.”[1]

Kuhusu tisa Yahyaa bin Sa´iyd al-´Attwaar amenihadithia, kutoka kwa Thawr bin Yaziyd, kutok kwa Khaalid bin Ma´daan, kutoka kwa bwana mmoja, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Uislamu unazo alama za ardhi na ishara za barabara kama zilivyo za barabara. Miongoni mwazo ni kumwamini Allaah na kutomshirikisha na chochote, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan, kuhiji Nyumba, kuamrisha mema, kukataza maovu, kuwasalimia familia yako pindi unapoingia kwao na kuwasalimia watu pindi unapokutana nao. Yule mwenye kuacha chochote katika hayo basi ameacha sehemu ya Uislamu na yule mwenye kuyaacha basi ameupa Uislamu mgongo.”

Wajinga wanadhani kwamba Hadiyth hizi ni zenye kugongana kwa sababu ya kutofautiana kwa idadi ya matendo yake. Himdi zote zinarejea kwa Allaah ziko mbali kabisa na kutofautiana. Nimekwishakujuza kwamba matendo, faradhi na imani vilishushwa hatua kwa hatua. Kila kulipokuwa kunashuka faradhi basi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaiongeza juu ya imani. Na kila ambapo Allaah anaifanya upya faradhi basi anaiongeza katika zile zilizotangulia mpaka idadi ikazidi mambo sabini. Abu Ahmad az-Zubayriy ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan bin Sa´iyd, kutoka kwa Suhayl bin Abiy Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Imani ni tanzu sabini na kitu. Ya juu yake ni “Laa ilaaha illa Allaah” na ya chini yake ni kuokota chenye kudhuru kutoka njiani.”

Idadi iliyoongezeka haipo katika ile nambari ya idadi ilizotangulia; ile ya kwanza iliotajwa ni nguzo na misingi na hizi zilizokuja nyuma ni matawi yenye kuzidi juu ya hizo nguzo.

[1] Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim, ambaye pia kaipokea.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 19-25
  • Imechapishwa: 14/05/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy