Hapa ndipo walipokosea wale wenye kuona kuwa imani ni kwa kutamka peke yake. Waliposikia Allaah amewaita “waumini” ndipo wakaona kuwa imani zao ni kamilifu. Pia wamezifahamu makosa Hadiyth pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesem:

“Imani ni kumwamini Allaah… “[1]

na Hadiyth ya yule bwana ambaye alikuwa anataka kumwacha mjakazi muumini asiyekuwa mwarabu ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamrisha amwache huru na akamwita kuwa ni muumini[2]. Kama nilivokwambia haya yanajulisha juu ya kuingia kwao ndani ya imani na kukubali na kusadikisha ile sehemu ya imani iliokuwa imekwishateremshwa kipindi hicho. Kwani ilikuwa ikiteremka hatua kwa hatua kama ilivyokuwa inashuka imani. Dalili ya hayo niyasemayo yako katika Kitabu cha Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika Qur-aan ni pamoja na maneno Yake:

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ

“Na inapoteremshwa Suurah, basi miongoni mwao wako wanaosema: “Nani kati yenu [Suurah] hii imemzidishia imani?” Ama wale walioamini huwazidishia imani nao wanafurahia.”[3]

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا

“Hakika si vyenginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake basi huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea. Ambao wanasimamisha swalah na hutoa sehemu ya vile Tulivyowaruzuku; – hao ndio waumini wa kweli.”[4]

Huoni kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hakuteremsha imani kwa mkupuko mmoja kama ambavo hakuteremsha Qur-aan kwa mkupuko mmoja? Hii ndio dalili ndani ya Qur-aan. Kama imani ingelikuwa imekamilika kwa kule kukiri basi kuzidi kungelikuwa hakuna maana yoyote. Wala kusingekuwa na maana yoyote kule kuitaja.

[1] Anaashiria Hadiyth ya Jibriyl iliyotolewa na al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah na Muslimi peke yake kupitia kwa Ibn ´Umar, kutoka kwa ´Umar. Tazama Hadiyth 119 katika “Kitaab-ul-Iymaan” cha Ibn Abiy Shaybah.

[2] Anaashiria Hadiyth ya Mu´aawiyah bin al-Hakam as-Sulamiy ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuuliza mjakazi: “Allaah yuko wapi?” Imepokelewa na Muslim. Tazama 84 “Kitaab-ul-Iymaan” cha Ibn Abiy Shaybah.

[3] 09:124

[4] 8:2-4

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 14/05/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy