06. Dalili zinahusiana na yule asiyeswali, na si yule anayekanusha uwajibu wake

Mtu akiuliza kama dalili hizi zilizotajwa zinazofahamisha ukafiri wa asiyeswali si zinaweza kufasiriwa kwamba ni yule ambaye anakanusha uwajibu wake, nasema kuwa hilo haliwezekani kutokana na sababu mbili:

1- Hii itakuwa na maana ya kufuta ule wasifu uliozingatiwa na Shari´ah na kufungamanisha hukumu nao. Shari´ah imefungamanisha hukumu na kule kuacha na sio kukanusha. Udugu wa dini umethibitishwa kwa kusimamisha swalah na sio kwa kule kukubali uwajibu wake. Allaah (Ta´ala) hakusema:

“Wakitubu na wakakubali uwajibu wa swalah na wakatoa zakaah, basi ni ndugu zenu katika dini.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusema:

“Baina ya mtu na shirki na kufuru ni kukanusha uwajibu wa swalah.”

“Ahadi iliyopo baina yetu na wao ni kukubali uwajibu wa swalah. Atakayekanusha uwajibu wake amekufuru.”

Lau haya ndio yangelikuwa makusudio ya Allaah (Ta´ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi uelewa huo ungelikuwa ni kinyume na ile bayana iliyokuja katika Qur-aan. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ

“Tumekuteremshia Kitabu kinachobainisha kila kitu.”[1]

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao.”[2]

2- Hiyo itakuwa na maana ya kuzingatia wasifu ambao Shari´ah haikufungamanisha hukumu nao. Kukanusha uwajibu wa swalah tano ni kufuru ikiwa huyo mkanushaji hapewa udhuru kwa ujinga wake, ni mamoja akaswali au asiswali. Lau ataswali vipindi vitano na akatekeleza sharti, nguzo, mambo ya wajibu na mambo yaliyopendekezwa ya swalah, ni kafiri hata kama ataswali. Kwa hiyo linafahamisha kuwa si sahihi kuzifasiri dalili kwamba zinahusiana na yule asiyeswali kwa sababu anakanusha uwajibu wake. Linafahamisha vilevile kwamba yule asiyeswali ni kafiri na anatoka katika Uislamu. Hilo limetajwa wazi katika Hadiyth ambayo Ibn Abiy Haatim amepokea katika “as-Sunan” yake kupitia kwa ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuusia: “Tusimshirikishe Allaah na chochote na tusiache swalah kwa kukusudia. Atayeacha swalah kwa kukusudia ametoka katika dini.””

Jengine ni kwamba endapo tutafasiri kwamba dalili zinahusiana na yule asiyeswali kwa kukanusha uwajibu wake, ule umaalum uliyotajwa katika dalili usingelikuwa na faida yoyote. Kwa sababu hukumu hii ni yenye kuenea juu ya zakaah, swawm na hajj. Atakayeacha kimoja katika hayo hali ya kukanusha uwajibu wake basi ni kafiri ikiwa sio mwenye kupewa udhuru kwa sababu ya ujinga wake.

Kama ambavyo haya yanaendana na dalili za kiwahyi na za kimapokezi, vilevile zinaendana na dalili za kiakili na za kinadharia. Ni vipi mtu atakuwa muumini pamoja na kuwa ameacha swalah ambayo ndio nguzo ya dini na ambayo imeamrishwa kiasi cha kwamba kila muumini mwenye busara anakimbilia kuitekeleza na matishio juu ya kuiacha kiasi cha kwamba kila muumini mwenye busara anachelea kuiacha na kuipuuza? Kwa hiyo yule asiyeswali hana imani.

[1] 16:89

[2] 16:44

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm Taarik-is-Swalaah, uk. 8-10
  • Imechapishwa: 22/10/2016