05. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya Vitabu na Mitume III


5- Nguzo ya tano: Kuamini siku ya Mwisho: Nako ni kule kufufuliwa baada ya kufa. Kwa sababu dunia ni nyumba ya matendo na Aakhira ni nyumba ya malipo. Dunia ni shamba kwa ajili ya Aakhirah. Kwa hivyo ni nyumba ya matendo na hakuna malipo ndani yake. Vilevile Aakhirah ni nyumba ya malipo na hakuna matendo ndani yake. Kwa hivyo ni lazima kuamini siku ya Mwisho. Yule asiyeamini siku ya Mwisho ni kafiri. Amesema (Ta´ala):

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ

”Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu! Bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda.”[1]

Ee mwanadamu ambaye unaishi katika dunia hii; unakula, unakunywa, unakufuru na unaasi kana kwamba hakuna mbele yako kufufuliwa, hesabu na malipo. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameifanya Aakhirah kwa ajili ya malipo. Huu ni uadilifu Wake (Subhaanah) ya kwamba hapotezi matendo ya watendaji. Anamlipa kila mmoja kutokana na matendo yake:

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ

“Je, mlidhania kwamba Sisi Tulikuumbeni bila kusudio mcheze tu na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?”[2]

Lau kusingelikuweko jambo la kufufuliwa basi kuumbwa kungekuwa ni mchezo tu, jambo ambalo Allaah (Subhaanah) ametakasika kutokamana nalo.

6- Nguzo ya sita: Kuamini Qadar. Qadar ni siri ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Qadar ni yale aliyokadiria Allaah katika mambo yaliyokuweko na yatayokuweko mpaka kisimame Qiyaamah. Kalamu imeandika makadirio na imeyaandika katika Ubao uliohifadhiwa yatayokuweko mpaka siku ya Qiyaamah. Hakutokei kitu isipokuwa kwa Qadar:

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

”Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa Qadar.”[3]

Kwa hivyo mambo sio burebure. Bali ni yamekwishakadiriwa tokea hapo kabla:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa upo katika Kitabu, kabla hatujautokezesha.”[4]

Maneno Yake:

“Kitabu”

ni Ubao uliohifadhiwa. Maneno Yake:

قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا

“… kabla hatujautokezesha.”

Bi maana kabla ya kuumba.

Zipo ngazi nne juu ya kuamini Qadar:

Ya kwanza: Kuamini elimu ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) ya milele, daima na iliyokizunguka kila kitu. Kwa msemo mwingine ni kwamba tunaamini kuwa Allaah alikijua kila kitu; alijua yaliyokuweko na yatayokuweko.

Ya pili: Kuamini kuwa Allaah ameandika kwenye Ubao uliohifadhiwa yatayokuweko hadi siku ya Qiyaamah.

Ya tatu: Matakwa na utashi. Anayotaka Allaah, huwa, na asiyoyataka, hayawi.

Ya nne: Kuumba vitu ndani ya wakati wake uliopangiwa. Kila kitu ndani ya wakati wake na kila kitu ndani ya kipindi chake alichokadiria Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Kwa hivyo ni lazima kuamini ngazi hizi nne:

– Ngazi ya ujuzi.

– Ngazi ya uandishi.

 – Ngazi ya utashi.

– Ngazi ya uumbaji.

Huku ndio kuamini mipango na makadirio.

[1] 64:07

[2] 23:115

[3] 54:49

[4] 57:22

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 20-21
  • Imechapishwa: 02/03/2021