06. Kuamini majina na sifa za Allaah ni katika kumwamini Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Katika kumwamini Allaah kunaingia vilevile kuamini yale Aliyojisifu Mwenyewe katika Kitabu Chake na kupitia kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtu anatakiwa kufanya hivo bila ya kupotosha wala kukanusha.”

MAELEZO

Alipobainisha nguzo za imani amebainisha yale yanayoingia katika sehemu ya kwanza ambayo ni kumwamini Allaah ya kwamba kunaingia vilevile kuamini majina na sifa za Allaah. Yule mwenye kukanusha majina na sifa za Allaah si mwenye kumwamini Allaah imani ya kweli. Hii ni Radd kwa wakanushaji ambao wamekanusha majina na sifa za Allaah kwa sababu wao hawaamini majina na sifa za Allaah.

Miongoni mwa kumwamini Allaah mtu anatakiwa vilevile kuamini majina na sifa za Allaah zilizotajwa katika Qur-aan na Sunnah.

Mtu anatakiwa kufanya hivo bila ya kupotosha – Kupotosha ni kule kubadilisha. Ni ima kubadilisha matamshi au kubadilisha ile maana. Huku ndio kupotosha.

Kupotosha matamshi inakuwa ima kwa kuzidisha ndani yake au kupunguza. Kwa mfano “kulingana” (Istiwaa) wamesema kuwa ni “kutawala” (Istawlaa). Huku ni kupotosha matamshi. Wamezidisha herufi.

Miongoni mwa kupotosha maana ni kufasiri kwamba maana ya kulingana ni kutawala, kufasiri mkono wa Allaah kwamba ni uwezo wa Allaah na uso wa Allaah kwamba ni dhati ya Allaah. Huku ni katika kuyakengeusha maneno ya Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ

“… wanayapotosha maneno kuyatoa mahali pake.”[1]

Wala kukanusha – Kukanusha ni kupinga majina na sifa za Allaah na kumtokomeza Allaah kutokamana navyo.

[1] 04:46

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 22
  • Imechapishwa: 02/03/2021