Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tunaonelea kuwa Sunnah imejengwa juu ya kushikamana na yale waliyokuwemo Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwaiga, kujiepusha na Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

MAELEZO

Ni wajibu kwa kila mtu kutambua kuwa anawajibika kumfuata na kumtii Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye kaamrisha hilo:

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ

”Sema: “Mtiini Allaah na mtiini Mtume.””[1]

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ

”Kile anachokupeni Mtume, basi kichukueni, na kile anachokukatazeni, basi kiacheni. Mcheni Allaah; hakika Allaah ni mkali wa kuadhibu.”[2]

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

”Haiwi kwa muumini mwanamume na wala kwa muumini mwanamke pindi anapohukumu Allaah na Mtume Wake jambo lolote iwe wana khiyari katika jambo lao; na anayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika amepotoka upotofu wa wazi.”[3]

Mja wa Allaah! Ndani ya kaburi lako na siku ya Qiyaamah utaulizwa kama ulimfuata, ulimsadikisha na ulimwamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَنَسْأَلَنَّ الَّذِينَ أُرْسِلَ إِلَيْهِمْ وَلَنَسْأَلَنَّ الْمُرْسَلِينَ فَلَنَقُصَّنَّ عَلَيْهِم بِعِلْمٍ ۖ وَمَا كُنَّا غَائِبِينَ

“Basi bila ya shaka Tutawauliza wale ambao waliopelekewa [Mitume] na tutawauliza Mitume. Kisha Tutawasimulia kwa ujuzi na hatukuwa wenye kukosekana.”[4]

al-Baraa´ bin ´Aazib ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mja anapolazwa ndani ya kaburi lake na marafiki zake wakamwacha na akasikia nyayo za viatu vyao, hujiwa na Malaika wawili. Mmoja wao anaitwa Nakiyr na mwingine anaitwa Munkar. Watamkaza na kumwambia: “Mola wako ni nani? Dini yako ni ipi? Ni nani huyu ambaye alitumwa kwenu?” Muumini atathibitishwa na Allaah na atajibu jibu la sawa: “Allaah ndiye Mola wangu, Uislamu ndio dini yangu na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Mtume wangu. Ametujia kwa dalili na uongofu ambapo tukamwamini na kumfuata.” Kafiri, au mnafiki, atasema: “Eeh, eeh. Sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema.” Atapigwa nyundo, lau mlima ungepigwa nayo basi ungeligeuka udongo. Atapiga ukelele wa hali ya juu utaosikiwa na viumbe wote isipokuwa tu majini na watu. Lau jini au mwanadamu angelisikia ukelele huo basi angelikufa.”[5]

Katika hajj ya kuaga alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Khutbah yake siku ya ´Arafah:

“Mtaulizwa juu yangu. Mtajibu nini?” Wakasema: “Tunashuhudia ya kwamba umefikisha.”[6]

Mwenye busara anatakiwa kuzingatia na kujiuliza kama kweli amemfuata yule aliyeamrishwa kumfuata. Au amewafuata watu wa matamanio wanaotaka kumpoteza?

Ninaiusia nafsi yangu mimi na nyinyi kufuata Sunnah na kujiepusha na Bid´ah. Bid´ah ni upotevu na maangamivu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha Bid´ah na kadhalika maimamu waongofu wamefanya hivo. Miongoni mwa matahadharisho ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni pale aliposema:

“Hakika yule atakayeishi zaidi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi kabisa. Hivyo basi jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Ziumeni kwa magego yenu. Ninakutahadharisheni na mambo ya kuzua, hakika kila kitachozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[7]

Amesema vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, atarudishiwa mwenyewe.”[8]

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Hivyo basi, watahadhari wale wanaokhalifu amri yake isije kuwapata fitnah au ikawapata adhabu iumizayo.”[9]

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu… “

Hii ni sehemu ya Hadiyth iliyotangulia kutajwa.

Vilevile inatupaswa tujue kuwa Bid´ah zote ni upotevu tofauti na baadhi ya waliosema kuwa kuna Bid´ah zilizo nzuri. Baadhi ya wengine wakasema kuwa Bid´ah imegawanyika katika zile hukumu tano. Wamekosea. Yale yanayohusiana tu na dini ndio huitwa “Bid´ah”, sio yale yanayohusiana na mambo ya kidunia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuhusu upandaji wa mitende:

“Nyinyi ni wajuzi zaidi juu ya mambo ya dunia yenu kuliko mimi.”[10]

Vinavyotumiwa kwa ajili ya mambo ya kidunia haviitwi kuwa ni “Bid´ah”, isipokuwa ni kitu kinachotumiwa kwa ajili ustawi unahitajia hivo. Neno “Bid´ah” linatumiwa katika mambo ya ´ibaadah na ya dini.

[1] 24:54

[2] 59:07

[3] 33:36

[4] 07:06-07

[5] Ahmad (4/287) na Abuu Daawuud (4753). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Mishkaah” (131).

[6] Muslim (1218).

[7] Abuu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[8] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[9] 24:63

[10] Muslim (2363).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 70-73
  • Imechapishwa: 27/01/2017