04. Anaona damu kinyume na muda aliyozowea kupata hedhi

Swali 4: Ni ipi hukumu ikiwa mwanamke amezowea kupata ada yake ya mwezi siku nane au saba kisha ikatokea si chini ya mara moja ada yake ikaendelea zaidi ya muda aliyozowea?

Jibu: Ikiwa mwanamke amezowea kupata hedhi kwa muda wa siku sita au saba kisha muda huu ukarefuka na ikawa siku nane, tisa, kumi au kumi na moja, basi atakaa na asiswali mpaka atwahirike kwanza. Hilo ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuweka muda maalum wa hedhi. Isitoshe Allaah (Ta´ala) amesema:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى

“Wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara.”[1]

Muda wa kuwa damu hii bado ipo basi mwanamke abaki katika hali yake mpaka asafike kwanza, kisha ataoga na kuswali.

Mwezi wa kufuata ada yake ikimjia hali ya kuwa imepungua masiku hayo, basi ataoga akiwa ametwahirika hata kama si kwa ule muda uliotangulia. Muhimu ni kwamba muda wa kuwa mwanamke bado yuko na hedhi basi asiswali. Ni mamoja hedhi hiyo imeafikiana na muda uliotangulia, imezidi au kupungua juu yake. Baada ya hapo akitwahirika ataswali.

[1] 02:222

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 60 su-aal wa jawaab fiy Ahkaam-il-Haydhw, uk. 9-10
  • Imechapishwa: 11/06/2021