03. Matahadharisho ya Mtume kuzua katika dini


Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ambazo ni Swahiyh akitahadharisha Bid´ah na kuweka wazi kuwa ni upotevu kwa lengo la kuwazindua Ummah kuwaonesha ukhatari wake na kuwaogopesha kuyavumbua. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo basi atarudishiwa.”[1]

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Yeyote atakayefanya kitendo ambacho hamna ndani yake dini yetu atarudishiwa.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika Khutbah zake siku ya Ijumaa:

“Amma ba´d; hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa. Kila Bid´ah ni upotofu.”[2]

Katika Sunan kumepokelewa kupitia kwa al-´Arbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutolea mawaidha makali ambayo yalitikisa mioyo yetu na macho yetu yakatiririka machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga, basi tuusie.” Ndipo akasema: “Ninakuusieni usikivu na utiifu hata kama mtatawaliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo bara bara na mziume kwa magego. Tahadharini na mambo ya kuzua! Hakika kila kitakachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”

Hadiyth zenye maana kama hii ni nyingi.

[1] al-Bukhaariy (2550) na Muslim (1718).

[2] Muslim (867).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 23/01/2022