Suala la tatu: Kipindi cha I´tikaaf, mapendekezo yake na yanayoruhusu kwa anayefanya I´tikaaf

1- Kipindi cha I´tikaaf na wakati wake

Ni nguzo ya I´tikaaf kubaki msikitini kwa kiwango cha muda fulani. Kusipotokea kitendo cha kubaki na kukaaa msikitini basi I´tikaaf inakuwa haijafungika. Wanachuoni wametofautiana kuhusu uchache wa muda wa I´tikaaf. Maoni sahihi – Allaah akitaka – ni kwamba I´tikaaf haina kiwango chache cha chini. I´tikaaf inasihi kwa muda kiwango fulani ijapo utakuwa mchache. Pamoja na kwamba bora I´tikaaf isipungue mchana na usiku mmoja. Haijapokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka kwa mmoja katika Maswahabah kukaa I´tikaaf chini ya hapo.

Kipindi bora cha kukaa I´tikaaf ni zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliyotangulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaa I´tikaaf katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan mpaka Allaah alipomfisha[1]. Akikaa I´tikaaf mbali na kipindi hicho ni jambo linalofaa licha ya kuwa linakwenda kinyume na ambalo ni bora zaidi.

Ambaye amenuia kukaa I´tikaaf katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan basi ataswali Fajr asubuhi ya tarehe 21 katika ule msikiti ambao amenuia kukaa I´tikaaf ndani yake. Baada ya hapo ataanza I´tikaaf yake. I´tikaaf itamalizika kwa kuzama jua katika ile siku ya mwisho ya Ramadhaan.

[1] al-Bukhaariy (2020) na Muslim (1172).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 169
  • Imechapishwa: 02/05/2021