Suala la pili: Sharti za I´tikaaf

I´tikaaf ni ´ibaadah ambayo iko na sharti ambazo haisihi isipokuwa kwazo. Nazo ni zifuatazo:

1- Yule mwenye kufanya I´tikaaf anatakiwa awe muislamu, mwenye uwezo wa kupambanua na mwenye akili. Kwa msemo mwingine ni kwamba I´tikaaf haisihi kwa kafiri, mwendawazimu wala mtoto asiyeweza kupambanua. Jambo la kubaleghe na ujana ni vitu viwili ambavyo havikuwekewa sharti. Hiyo ina maana kwamba I´tikaaf inasihi kwa ambaye hajabaleghe muda wa kuwa ana uwezo wa kupambanua. Vivyo hivyo kwa msichana.

2- Nia. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika si venginevyo matendo yanalipwa kutegemea na nia.”[1]

Kwa hivyo mkaaji I´tikaaf anatakiwa kulazimiana na mahali pake kwa nia ya kujikurubisha na kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall).

3- I´tikaaf inatakiwa kukaliwa msikitini. Amesema (Ta´ala):

وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ

“… na hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa I’tikaaf  misikitini.”[2]

Aidha kitendo chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa vile alikuwa akikaa I´tikaaf msikitini na haikupokelewa kutoka kwake kwamba aliikaa I´tikaaf kwenginepo.

4- Msikiti ambao mtu anakaa I´tikaaf kuwe kunaswaliwa swalah ya mkusanyiko. Hilo ni kwa sababu kipindi kile cha I´tikaaf kinakumbana na vile vipindi vitano vya swalah na wakati huohuo swalah ya mkusanyiko ikawa ni lazima kwa yule mfanyaji I´tikaaf. Kwa sababu kufanya I´tikaaf ndani ya msikiti ambao hakuswaliwi swalah ya mkusanyiko kutapelekea kuacha kuswali swalah ya mkusanyiko ambayo inamlazimu au itampelekea yule mkaaji kutoka kila wakati, jambo ambalo linapingana na malengo ya I´tikaaf.

Kuhusu mwanamke inasihi I´tikaaf yake katika kila msikiti. Ni mamoja msikiti kunaswaliwa swalah ya mkusanyiko au hakuswaliwi. Hali hiyo ni pale ambapo I´tikaaf yake haipelekei katika fitina yoyote. Ikiwa I´tikaaf yake itapelekea katika fitina basi atazuiwa.

Bora ni kukaa I´tikaaf katika msikiti ambao kunaswaliwa swalah ya ijumaa. Lakini hilo sio sharti la I´tikaaf.

5- Kusafika kutokamana na hadathi kubwa. Hiyo ina maana kwamba haisihi I´tikaaf ya aliye na janaba, mwenye hedhi na aliye na damu ya uzazi. Kwa sababu haifai kwa watu hawa kukaa na kubaki msikiti.

Kufunga sio sharti ya I´tikaaf. Imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwamba ´Umar alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika mimi katika kipindi cha kikafiri niliweka nadhiri ya kukaa I´tikaaf ndani ya msikiti Mtakatifu.” Akasema: “Tekeleza nadhiri yako.”[3]

Ingelikuwa kumeshurutishwa kufunga basi isingesihi kukaa I´tikaaf wakati wa usiku. Kwani usiku hakuna kufunga. Isitoshe hizo ni ´ibaadah mbili tofauti. Kupatikana kwa moja hakushurutishi kupatikane kwa nyingine.

[1] al-Bukhaariy (01) na Muslim (1907).

[2] 02:187

[3] al-Bukhaariy (2032) na Muslim (1656).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 167-168
  • Imechapishwa: 02/05/2021