02. Baadhi ya sifa za Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na makatazo ya waislamu kutofautiana


Kundi hilo limeitwa ”lililookoka” kwa sababu limeokoka kutokamana na Moto. Mapote yote yako Motoni isipokuwa kundi hili tu. Kwani lenyewe limesalimika kutokamana na Moto. Hizi ndio sifa zake:

1- Ni lenye kuokoka.

2- Wao ni Ahl-us-Sunnah ambao wanazitendea kazi Sunnah ambayo ni njia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kunamaanishwa Qur-aan na Hadiyth Swahiyh. Yale aliyokuwemo juu yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama alivosema:

”Ni wale wataokuwa katika mfano wa yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

Hawakufuata madhehebu ya Jahmiyyah, Mu´tazilah, Khawaarij au wengineo katika mapote. Wao wamefuata mfumo wa Ahl-us-Sunnah ambao ni kushikamana barabara na Sunnah.

3- al-Jamaa´ah. Wameitwa “al-Jamaa´ah” kwa sababu wamekusanyika juu ya haki na hawana tofauti. Hawatofautiani katika ´Aqiydah zao. ´Aqiydah yao ni moja ingawa ni wenye kutofautiana katika mambo ya ki-Fiqh na mambo ya mataga ambayo wanajitahidi, jambo ambalo halidhuru. Tofauti katika mambo ya Fiqh haidhuru. Kwa sababu yametokana na Ijtihaad. Ijtihaad za watu zinatofautiana. Watu hawako katika kiwango kimoja katika upeo wa Ijtihaad. Kuhusu ´Aqiydah haikubali Ijtihaad. Bali ni lazima iwe moja kwa sababu ni kitu cha kukomeka. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ

“Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja Nami ni Mola wenu, basi niabuduni.”[1]

Ummah huu ni mmoja na haukubali mambo ya tofauti. Unatakiwa kumwabudu Allaah mmoja. Katika Aayah nyingine imekuja:

وَإِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ فَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ زُبُرًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

“Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja Nami ni Mola wenu, basi Nicheni. Lakini wakalivunja jambo lao baina yao makundi mbalimbali, kila kundi kwa waliyokuwa nayo linafurahia.”[2]

Amewasema vibaya wale wenye kutofautiana. Kwa sababu tofauti katika ´Aqiydah haijuzu. Allaah amewaamrisha wawe Ummah mmoja lakini hata hivyo wakamuasi:

فَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ زُبُرًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

”Lakini wakalivunja jambo lao baina yao makundi mbalimbali, kila kundi kwa waliyokuwa nayo linafurahia.”

Bi maana kitabu. Hayo yamesemwa na Qataadah na Mujaahid[3]. Ikawa kila mmoja ana kitabu chake na kila mmoja ana imani yake na hatimaye imani ya huyu ikawa sio imani ya yule:

كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

“Kila kundi kwa waliyokuwa nayo linafurahia.”

Kila mmoja anaona kuwa yeye ndiye yuko katika haki na wengine wako katika batili. Hawakuwa wanaona kurejea katika Qur-aan na Sunnah, kama alivosema (Ta´ala):

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

“Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho.”[4]

Bali kila mmoja anasema kuwa yeye peke yake ndiye yuko katika haki:

كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

“Kila kundi kwa waliyokuwa nayo linafurahia.”

Isitoshe anakuwa ni mwenye kukinaika juu ya yale anayoyafanya. Sivyo tu bali anayashabikia pia. Haoni kuwa maneno yake yanaweza kuingiliwa na kukosea na kupatia.

[1] 21:92

[2] 23:52-53

[3] Athar ya Qataadah ameipokea ´Abdur-Razzaaq katika ”Tafsiyr yake” (03/46) na at-Twabariy katika ”Tafsiyr yake” (18/29).

Athar ya Mujaahid ameipokea vilevile at-Twabariy katika ”Tafsiyr yake” (18/30). Tazama “ad-Durar al-Manthuur” (06/103).

[4] 04:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 25/03/2021