03. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya Allaah na Malaika Wake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, kufufuliwa baada ya kufa na kuamini Qadar kheri na shari yake.”

MAELEZO

Hii ndio misingi na nguzo za imani. Shaykh anayaamini. Nayo ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, kufufuliwa baada ya kufa na kuamini Qadar kheri na shari yake. Kama ilivyo katika Hadiyth ya Jibriyl wakati alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mbele ya Maswahabah zake ambapo akamuuliza: “Nijuze juu ya imani?” Akasema:

“Imani ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, kufufuliwa baada ya kufa na kuamini Qadar kheri na shari yake.”[1]

Wanachuoni wamesema kuwa hizi ndio nguzo za imani. Imani ina nguzo na vilevile ina tanzu. Nguzo zake ni sita na tanzu zake “Ni tanzu sabini na kitu. Ya juu yake ni “Laa ilaaha illa Allaah” na ya chini yake ni kuokota chenye kudhuru kutoka njiani. Hayaa ni tanzu ya imani.”[2]

Imani ina tanzu nyingi sana. Ama nguzo zake – bi maana misingi yake ambayo inasimama juu yake – ni nguzo sita:

1- Nguzo ya kwanza: Kumwamini Allaah, na ndio msingi. Kumwamini Allaah ndani yake kumekusanya aina tatu za Tawhiyd; Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na Tawhiyd al-Asmaa´ was-Swifaat.

2- Nguzo ya pili: Kuwaamini Malaika: Inatakiwa kuamini kwamba wao ni waja miongoni mwa waja wa Allaah (Ta´ala). Hawamtangulii kwa kauli nao kwa amri Yake ni wenye kuitekeleza. Allaah amewaumba kutokana na nuru. Wao ni katika ulimwengu uliofichikana ambao hatuwaoni. Lakini hata hivyo tunawaamini. Allaah amewafanya kuwa aina mbalimbali. Kila aina ya Malaika wana kazi wanaoitekeleza katika ulimwengu huu. Miongoni mwao wako wenye kudhibiti ambao wanayadhibiti matendo ya wanaadamu na kuyaandika:

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ كِرَامًا كَاتِبِينَ يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ إِنَّ الْأَبْرَارَ لَفِي نَعِيمٍ

“Hakika juu yenu wako wenye kuhifadhi; watukufu wanaoandika, wanajua yale mnayoyafanya.”[3]

Katika wao wako wenye kubeba ´Arshi na miongoni mwao yuko mwenye kazi ya Wahy ambaye ni Jibriyl (´alayhis-Salaam). Miongoni mwao wako wenye kazi ya kuteremsha mvua ambaye ni Mikaaiyl. Miongoni mwao wako wenye kazi ya kufisha ambaye ni Malaika wa mauti. Huandamana na Malaika wengine wa mauti. Miongoni mwao kuko aina zengine ambazo hakuna azijuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَمَا يَعْلَمُ جُنُودَ رَبِّكَ إِلَّا هُوَ

“Hakuna anayeua majeshi ya Mola wako isipokuwa Yeye pekee.”[4]

Wanajeshi wa Allaah ni wengi.

[1] Muslim katika “as-Swahiyh” yake (08) kupitia kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Vilevile ameipokea al-Bukhaariy (50, 4777), Muslim (09, 10) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] Muslim katika ”as-Swahiyh” yake (35) kupitia kwa Abu Hurayra (Radhiya Allaahu ´anh).

[3] 82:12-13

[4] 74:31

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 01/03/2021