Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

669- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiitangulizie Ramadhaan kwa kufunga siku moja au mbili, isipokuwa mtu ambaye alikuwa akifunga swawm. Basi aiendeleze.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

670- ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Yule mwenye kufunga siku ambayo inatiliwa shaka basi amemwasi Abul-Qaasim (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy ikiwa na cheni ya wapokezi pungufu na wale Watano wameipokea ikiwa na cheni ya wapokezi ilioungana. Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan wameisahihisha.

MAELEZO

Kufunga ni kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall) kwa kuacha kula, kunywa, jimaa na mambo mengine yanayofunguza kuanzia pale ambapo kunapambazuka alfajiri mpaka pale ambapo jua huzama. Mtu anafanya hayo kwa kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall) na kutekeleza utiifu Wake.

Kufunga ni moja katika nguzo tano za Uislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kuhiji Nyumba ya Allaah tukufu na kufunga Ramadhaan.”[3]

Allaah (Ta´ala) amefaradhisha swawm katika mwaka wa 02. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafunga Ramadhaan tisa. Mwanzoni kufunga mtu alikuwa na chaguo; atakaye anafunga na atakaye anatoa chakula. Baada ya hapo ikawa ni lazima kufunga Ramadhaan nzima.

[1] al-Bukhaariy (1914) na Muslim (1082).

[2] al-Bukhaariy (27/3), Abu Daawuud (2334), at-Tirmidhiy (686), an-Nasaa’iy (2188), Ibn Maajah (1645), Ibn Khuzaymah (1914) na Ibn Hibbaan (3594).

[3] al-Bukhaariy (8) na Muslim (16).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymîn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/405-406)
  • Imechapishwa: 21/04/2020