Watu wa familia ya Mtume ni safina ya Nuuh?

Swali: Je, si miongoni mwa sababu za kucheleweshwa kwetu – ambazo Mashaykh hawajazitaja – kwamba tumewatawalisha juu yetu watu wasiofaa na hatukufuata maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watu wa familia yangu ni kama safina ya Nuuh. Yule anayeipanda basi amesalimika, na anayeiacha basi ameangamia”?

Sisi leo kwa muda mrefu tumekuwa tukizama.

Jibu: Haya ni miongoni mwa maneno ya Shiy´ah. Hii ni Hadiyth batili, iliyozuliwa na haina msingi. Watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si wao wenyewe safina ya uokovu. Wao wana haki ya kushauriwa, kutendewa wema, kufundishwa wajinga wao na kusamehewa makosa yao pale inapowezekana kuvumilia na mengine katika haki alizozikumbusha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini wao si safina ya uokovu. Safina ya kweli ni Qur-aan na Sunnah. Mwenye kushikamana navyo atasalimika, na mwenye kuviacha ataangamia. Watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wako wa haki na wako wa batili. Miongoni mwao ni pamoja na Abu Twaalib ambaye ni katika watu wa Motoni na Abu Lahab ambaye ni katika watu wa Motoni. Miongoni mwao ni ´Aliy ambaye nik katika watu wa Peponi, wanawe kama al-Hasan, al-Husayn, Muhammad bin ´Aliy na wengine katika kizazi chema cha watu wa familia ya Mtume walio juu ya uongofu na utiifu. Walio bora kuliko wao ni Abu Bakr as-Swiddiyq, ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anhumaa), pamoja na ´Uthmaan bin ´Affaan na makhaliyfah waongofu. Hao ni bora kuliko wengine. Wote hao wako katika njia ya uokovu na furaha, si watu wa familia tu. Kwa hivyo yeyote aliye sawa juu ya amri ya Allaah – ni mamoja awe ni mtu wa familia ya Mtume au siyo – basi yuko katika njia ya uokovu na ndani ya safina ya kweli. Yeyote anayeiacha njia ya utiifu kwa Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ataangamia, hata awe ni katika kizazi cha Manabii au wa watu wa nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hili ni jambo ambalo Shiy´ah na wafuasi wao wanapaswa kulijua.

Kadhalika kuna Hadiyth nyingine wanayotaja:

“Mimi ni mji wa elimu na ´Aliy ndiye mlango wake

Hii pia ni ya kutungwa. Maana yake ni kwamba hakuna elimu isipokuwa kupitia kwa ´Aliy pekee, jambo ambalo si sahihi. Vivyo hivyo Hadiyth isemayo:

“Watu wa familia yangu kama safina ya Nuuh”

imetungwa. Watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wale walio juu ya uongofu na utiifu, si wale waliopotoka na kuacha njia hiyo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1032/مدى-صحة-القول-اهل-بيتي-كسفينة-نوح
  • Imechapishwa: 19/01/2026