Wapeni bishara njema…

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Wape bishara njema wale walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo chini yake mito, kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni riziki husema “Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla” na wataletewa hali ya kuwa yanafanana; na watapata humo wake waliotwahirika nao humo ni wenye kudumu milele.”[1]

Baada ya kutaja malipo ya makafiri ndio akataja malipo ya waumini ambao ni wale wenye kutenda matendo mema. Huu ndio mwenendo wa Allaah ndani ya Qur-aan ambapo anakusanya kati ya kuvutia na kutia khofu ili mja awe mwenye kuvutiwa na wakati huohuo mwenye kuogopa, mwenye khofu na mwenye matarajio.

Ee Mtume na wale waliosimama nafasi yake! Wapeni bishara njema wale walioamini kwa mioyo yao na wakatenda matendo mema kwa viungo vyao. Kwa msemo mwingine imani yao ikasadikishwa kwa matendo mema. Matendo mema yamesifiwa kuwa ni ´mema` kwa sababu yenyewe ndio huzitengeneza hali za mja, mambo ya dini na ya dunia yake, maisha yake ya duniani na ya Aakhirah na kumwondoshea hali mbaya. Kwa mambo hayo anakuwa miongoni mwa waja wema ambao wanastahiki kuwa wakazi majirani wa Mwingi wa huruma katika Pepo Yake.

[1] 02:25

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 36
  • Imechapishwa: 28/05/2020