Swali: Unasemaje juu ya wale wanaotetea mfumo wa haki sawa (منهج الموازنة) na wanajengea hoja kwa maneno aliyoandika adh-Dhahabiy katika ”Siyaar A´laam-in-Nubalaa´?

Jibu: Nimeandika vitabu viwili kuhusu mada hii:

1 – Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy Naqd-ir-Rijaal wal-Kutub wat-Twawaaif.

2 – al-Mahajjah al-Baydhwaa’.

Aidha nimeraddi shubuha na uwongo wa ”an-Naswr al-´Aziyz ´alaar-Radd al-Wajiyz”. Nimejibu swali hili mara nyingi na ndio maana nimrejesha msomaji katika vitabu hivyo ili aweze kujua misingi ya Salaf. Vitabu hivyo vinajulisha juu ya ubatilifu wa mfumo huu uliyozuliwa na wa kipotofu. Naona kwamba hakuna mfumo ambao ni mbaya, wa kiovu na khatari kama huu. Unabomoa Qur-aan, Sunnah na elimu zote zilizowekwa katika Shari´ah. Sioni kuwa ni jambo lisilowezekana kuwa madajali wamezua mfumo huu wa kipekee kwa ajili ya kuwatetea wazushi na wapotofu.

Nitakupeni baadhi ya mifano; kitabu cha al-Bukhaariy ”adh-Dhwu´afaa´”. Ni kwa nini hakutaja mazuri ya wale watu ambao amewakosoa. Kwa mtazamo wa watu hawa al-Bukhaariy anakuwa mwenye kudhulumu na mtenda dhambi. Hivyo hatukubali kitabu chake hichi wala kitabu kingine alichoandika.

Ahmad bin Hanbal amewakosoa mamia ya watu bila kutaja mazuri walionayo. Yahyaa bin Ma´iyn, ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy, ´Aliy al-Madiyniy, al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah, ad-Daaraqutwniy, Ibn Hibbaan na Ibn Khuzaymah wamewakosoa watu pasi na kutaja mazuri walionayo. Wameandika vitabu kuhusu mada hii; al-Bukhaariy ameandika ”adh-Dhwu´afaa’”, an-Nasaa’iy ameandika ”adh-Dhwu´afaa’ wal-Matruwkiyn”, al-´Uqayliy ameandika ”adh-Dhwu´afaa’” na Ibn Hibbaan ameandika ”al-Majruwhiyn”. Someni na muangalie kama mtaona mfumo huu ndani yavyo.

Watu hawa wanajengea hoja na mwanahistoria adh-Dhahabiy. Wanahistoria wakati fulani wanachukulia usahali. Wanapoandika wasifu wakati fulani wanaandika mazuri na mabaya. Ni kwa nini hawataji vitabu vya adh-Dhahabiy ”Miyzaan-ul-I´tidaal”, ”ad-Diywaan”, ”al-Mughniy” na ”adh-Dhayl”? Watu hawa ni watu wa batili na watu wa shubuha. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema juu yao:

فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ

”Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotevu hufuata zile zisizokuwa wazi ili kutafuta fitina na kutafuta kuzipotosha.”[1]

Wanakengeusha Qur-aan, wanakengeusha Sunnah, wanakengeusha maneno ya Salaf. Sijaona Bid´ah ya khatari sana kushinda mfumo huu. Sijaona wazushi ambao ni khatari juu ya Uislamu kama watu hawa. Hawana jengine isipokuwa kutetea batili na ´Aqiydah zilizopotea. Unamkosoa mtu ambaye anawatukana Maswahabah na Mitume, wanakuuliza ni kwa nini hukutaja mazuri yake! Inapokuja kwa Ahl-us-Sunnah, hawataji chochote mazuri yao.

Kwa hivyo nawaombeni msome vitabu nilivyowatajia. Wanazuoni, akiwemo Ibn Baaz, al-Albaaniy na Ibn ´Utahymiyn, wamevisifu. Baadhi ya watu wamejirejea maoni yao na wakasema kuwa ukosoaji ikiwa ni kwa lengo la nasaha na kutahadharisha kwamba si lazima kutaja mazuri yao. Wako baadhi ambao wamefikia mpaka kusema kuwa kuna maafikiano ya jambo hilo. Mimi nawakosoa wazushi na wapotofu kwa lengo la nasaha na kutahadharisha, ni kwa nini wananitukana mimi na vitabu vyangu?

[1] 03:07

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 116-118
  • Imechapishwa: 26/12/2023