Vipi kuoanisha kati ya mwanamke kufanya kazi na kutulizana nyumbani kwake?

Swali: Ni ipi hukumu ya Kiislamu kuhusu mwanamke kufanya kazi katika elimu, tiba na uuguzi? Vipi inawezekana kukusanya jambo hilo na maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ

“Na tulizeni majumbani mwenu.”[1]?

Jibu: Mwanamke ana kazi zake na mwanaume ana kazi zake. Wanaweza kushirikiana katika baadhi ya kazi. Kila mmoja pia ana mambo anayoachiwa yeye pekee. Mwanamke anafanya kazi zinazomfaa kama kufundisha wanawake, kusimamia shule za wanawake, kuhudumia wanawake, kuwatibu wanawake na mengineyo katika kazi zilizoko katika uwanja wa wanawake. Pia pale kunapokuwa na haja ya kumhudumia mwanaume, kama kumuhudumia mgonjwa pale inapoonekana haja, kwa sharti la Hijaab, kujiepusha na machafu na kutokuwepo faragha. Haya yalifanyika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika baadhi ya vita, ambapo wanawake walikuwa wakiwapatia wagonjwa maji, wakiwahudumia majeruhi na walikuwa pamoja na waislamu katika kambi kwa ajili ya maslahi, wakiwa na Hijaab, sitara, heshima na kujiepusha na mambo ya shaka.

Kwa hiyo ikiwa mwanamke yuko katika mazingira ya Hijaab, kujiepusha na machafu na kuwa na heshima, na ikawa kunahitajika kumtibu mwanaume kwa kukosekana mwanaume wa kumpa huduma hiyo, basi hapana ubaya kumpatia dawa au kutengeneza dawa anayoihitaji. Vinginevyo uwanja wake ni uwanja wa wanawake katika tiba, elimu, uuguzi na mambo mengineyo. Mwanaume uwanja wake ni uwanja wa wanaume katika tiba, elimu na mambo mengineyo. Hiki ndio kilichowekwa katika Shari´ah na njia inayojulikana na yenye kufuatwa. Ikitokea haja ya mwanaume kumtibu mwanamke au mwanamke kumtibu mwanaume wakati wa haja, basi hapana ubaya kwa sharti la kuchunga Hijaab na kutokuwepo faragha, kama ilivyojulikana na kama ilivyokuja katika Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hili halipingani na maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ

“Na tulizeni majumbani mwenu.”

Aayah hii ina maana mbili:

1 – Kaeni majumbani mwenu na msitoke isipokuwa kwa haja na maslahi. Hili ndilo linaloonekana wazi. Mwanamke ni bora abaki nyumbani kwake isipokuwa kukiwepo haja. Akitoka kwa ajili ya swalah ya mkusanyiko hali ya kuwa na Hijaab na sitara, basi ni jambo lililokuwa likifanyika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vilevile walikuwa wakitoka kumtembelea mgonjwa, kutimiza haja kama kununua kitu sokoni na kadhalika. Hivyo ikiwa kutoka ni kwa haja na maslahi, basi hapana ubaya. Kilichotakiwa ni kubaki nyumbani pale ambapo hakuna haja ya kutoka.

2 – Makaa kwa heshima na utu wema. Kwa maana nyingine kaeni katika heshima, sitara na kujiheshimu na msipuuze haya wala msiwe watu wa kutofautisha mambo ya haya. Maana ya kwanza ndiyo yenye kutambulika, nayo ina maana ya kukaa nyumbani kwa amani na heshima. Hakuna upinzani kati ya maana hizi mbili.

[1] 33:33

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1111/حكم-عمل-المراة-في-التعليم-والطب-وغير-ذلك
  • Imechapishwa: 18/08/2026