Swali: Vipi kuhusu Bid´ah?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu Bid´ah:

“Tahadharini na mambo ya uzushi. Hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah. Kila Bid´ah ni upotevu. Kila upotevu ni Motoni.”

Mambo yakishakuwa hivo basi itambulike kuwa Bid´ah – ni mamoja iwe ule msingi wake au mwendelezo wake – anapata dhambi yule mwenye kuifanya. Kwa sababu mambo ni kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kila upotevu ni Motoni.”

Bi maana upotevu huu ni sababu inayopelekea mtu kuadhibiwa Motoni. Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameutahadharisha Ummah wake kutokamana na Bid´ah basi hilo linapelekea ya kwamba zenye kuharibu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kwa jumla na wala hakufanya maalum. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah.”

Jengine ni kwamba uhakika wa Bid´ah ni ukosoaji usiokuwa wa moja kwa moja juu ya Shari´ah ya Kiislamu. Kwa sababu maana yake ni kwamba Shari´ah bado haijatimia na kwamba uzushi huu ndio unaotimiza ile ´ibaadah aliyozua ambao anajikurubisha nao kwa Allaah, kama anavyodai. Hivyo basi tunamwambia:

“Hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah. Kila Bid´ah ni upotevu. Kila upotevu ni Motoni.”

Ni wajibu kwa watu kutahadhari Bid´ah zote na mtu asiabudu isipokuwa kwa yale Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walioyawekea Shari´ah ili aweze kuwa kiongozi wao wa kweli. Kwa sababu yule mwenye kufuata njia ya Bid´ah basi amemfanya mzushi huyu kuwa ndiye kiongozi wake katika Bid´ah hii badala ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (02/291)
  • Imechapishwa: 10/07/2017