00. Utangulizi wa “Sharh Hadiyth Jibriyl fiy Ta’liym-id-Diyn”

Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Sifa zote njema anastahiki Allaah ambaye ameridhia kwetu Uislamu kuwa ni dini na akatimiza kwetu neema na akaikimalisha dini. Na nakiri kwa moyo na kubaini kwa ulimi kwamba hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, Mmoja asiyemshirika, Mfalme wa kweli aliyewazi. Na nakiri kwa moyo na kubaini kwa ulimi kwamba Muhammad ni mja wake na Mtume wake, ambaye ametumwa na Allaah akiwa ni rehema kwa walimwengu wote. Ametekeleza amana, ameunasihi Umma na amefikisha ufikishaji uliowazi kabisa. Ewe Allaah mswalie a umsalimu na umbariki yeye na ahli zake na Swahabah zake na kila atakayefuata njia yake na akaongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.

Baada ya hayo yaliyokwishapita, hakika kwa muda mrefu nilikuwa nikitamani kuandika Sharh yenye kujitegemea ihusuyo Hadiyth ya Jibriyl ambayo imebeba ubainifu wa Uislamu, imani na ihsaan. Na alishasema Mtume ﷺ:

“Huyu ni Jibriyl amekujieni kuwafunza dini yenu.”

Na kwa fadhilah za Allaah hilo limewezekana pale ilipotoka hii Sharh mnamo mwaka 1424 H. Na kwa hakika wanazuoni wengi wamebainisha ukubwa na shani ya Hadiyth hii. Amesema al-Qaadhwiy ‘Iyaadhw (Rahimahu Allaah), kama ilivyokuja katika Sharh ya Imaam an-Nawawiy juu ya sahihi Muslim:

“Na Hadiyth hii imebeba sharh ya wadhifa nyingi za kiibada zilizo wazi na zilizofichikamana, ikiwemo mambo ya imani na matendo ya viungo na Ikhlaasw katika mambo ya siri pamoja na kujichunga kutokana na maafa ya matendo.” Mpaka kufikia kusema kwamba “Elimu zote za Shari’ah zinarejea katika hii Hadiyth na zimegawika kutokana na hiyo.” Akasema:

Na juu ya Hadiyth hii na vigawanyo vyake vitatu sisi tumeandika kitabu chetu tulichokiita:

“al-Maqaaswidil-Hisaan Fiy maa Yalzam-ul-Insaan.”[1]

Kwa kuwa hakuna chochote kati ya yale mambo ya wajibu na Sunnah na Raghaaibu pamoja na yaliyokatazwa na yaliyo makruhu kinachotoka katika vigawanyo vyake vitatu [Hadiyth hiyo] na Allaah ni Mjuzi zaidi.”

Na amesema Imam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah):

“Na fahamu ya kwamba Hadiyth hii imekusanya aina nyingi sana za elimu, maarifa, adabu na mengine yaliyo mazuri. Bali ndio msingi [mkuu wa] Uislamu kama tulivyosimulia kutoka kwa al-Qaadhwiy ‘Iyaadhw.”[2]

Na amesema Imam al-Qurtwubiy kama ilivyokuja katika “al-Fath”:

“Hadiyth hii inafaa kabisa iitwe mama wa Sunnah, kwa kufungamanikana ndani yake aina nyingi za elimu ya Sunnah.”[3]

Na amesema Ibn Daqiyq al-‘Iyd (Rahimahu Allaah) katika Sharh ya “al-Arba´iyn”:

“Mbele ya Sunnah [Hadiyth hii] ni sawa na mama. Kama ilivyoitwa Suurat-ul-Faatihah mama wa Qur-aan, kwa kukusanya kwake na kujumuisha maana zilizobebwa na Qur-aan.”

Na amesema Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) katika “Jaamiy´-ul-´Uluum wal-Hikam”:

“Ni Hadiyth Tukufu iliyosheheni kuisherehesha dini yote [kwa ukamilifu wake]. Na ndio maana akasema Mtume ﷺ mwishoni mwake:

“Huyu ni Jibriyl amekujieni akufunzeni dini yenu.”[4]

Na hilo ni baada ya kusherehesha daraja la Uislamu kisha daraja la Imani na Ihsani. Akayajaalia yote hayo kuwa ndio dini nzima.”

Na nimeipa jina:

”Sharh Hadiyth Jibriyl fiy Ta’liym-id-Diyn.”

Na namuomba Allaah (‘Azza wa Jall) anufaishe kupitia Sharh hii na awaafikishe watu wote katika kupata elimu yenye manufaa na kuifanyia kazi, kwani yeye ni Msikivu, Mwenye kujibu du´aa.

[1] (158/1)

[2] (1/160)

[3] (125/1)

[4] (97/1)