Swali: Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoingia nyumbani kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na akaona picha kwenye mapazia, hakuingia ndani mpaka zilipokatwa na kufanywa kuwa mito. Je, nimwigilize Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi ninapoingia sehemu kama hiyo?

Jibu: Hapana shaka kwamba kumwigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni miongoni mwa mambo ambayo Allaah ameamrisha. Amesema:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[1]

Unapoingia katika nyumba na ukakuta wametundika picha, basi unatakiwa kurudi nyuma na usiingie ndani. Lakini ikiwa unaweza kuongea na baba mwenye nyumba aondoshe picha hizo, basi mwombe afanye hivo na baada ya hapo ndio uingie ndani. Katika kufanya hivo kuna manufaa mawili:

1- Kuondoshwa kwa maovu hayo.

2- Kuitikia mwaliko.

Ama ikiwa unajua kuwa hatokubali na wala hatoondosha picha hizo, basi hapana shaka kwamba uongofu bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo usiingie ndani. Vivyo hivyo inahusu zile picha za familia, baba wa familia, mfalme, raisi au waziri; usiingie ndani muda wa kuwa kitu hicho kimetundikwa kwa juu.

[1] 33:21

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (26 A) Dakika: 15:30
  • Imechapishwa: 03/01/2021