Unayoruhusiwa kufanya na mwanamke kipindi cha hedhi

Swali: Mwanamume anaruhusiwa nini kutoka kwa mke wake katika siku za hedhi?

Jibu: Mwanamume anaruhusiwa kutoka kwa mke wake kila kitu isipokuwa tendo la ndoa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Fanyeni kila kitu isipokuwa tendo la ndoa.”

Wakati alipoambiwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba mayahudi hawakai na mwanamke anapokuwa katika hedhi majumbani, hawakai nao majumbani, hawali pamoja nao wala hawanywi nao. Ndipo akasema (´alayhis-Salaam):

”Fanyeni kila kitu isipokuwa tendo la ndoa.”

Allaah ameteremsha kuhusu hilo:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ

“Wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara, hivyo basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike.”[1]

Kwa maana ya jimaa.

Kuhusu kulala naye, kumkumbatia, kumbusu na mengineyo, hakuna tatizo lolote. Isipokuwa tendo la ndoa pekee.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuwa anakunywa kutoka kwenye chombo, kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakichukua na kuweka mdomo wake pale alipoweka mdomo wake. Pia alikuwa anakula kipande cha mfupa kilichokuwa na nyama, naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakichukua na kula katika sehemu aliyokula, ili kutuliza moyo wake, kumfariji na kumtania kwa upole (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 02:222

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30118/ماذا-يجوز-للرجل-من-زوجته-ايام-الحيض
  • Imechapishwa: 12/09/2025