Swali: Je, swalah ya Sunnah ya Fajr inalipwa ikiwa mtu ameikosa na pia Witr?

Jibu: Ndio, ikiwa mtu amekosa Sunnah ya Fajr, hulipwa baada ya swalah au baada ya kuchomoza jua na kupanda juu kidogo. Hii ndiyo Sunnah na hili ndilo bora zaidi. Kadhalika Witr ikiwa mtu ameikosa usiku, basi Sunnah ni kwamba muumini mwanamume na muumini mwanamke waiswali mchana kama alivyokuwa akiswali usiku. Lakini asiifanye witiri, aifanye iwe shufwa. Ikiwa alikuwa akiswali tano, basi aswali sita kwa Tasliym tatu. Ikiwa alikuwa akiswali tatu, basi aswali kwa Tasliym mbili. Ikiwa alikuwa akiswali saba, basi aswali Rak´ah nane kwa Tasliym nne na hivyo hivyo. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaposhughulishwa na maradhi au usingizi juu ya Witr ya usiku, huswali mchana Rak´ah kumi na mbili.”

Alikuwa mara nyingi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiswali Raka´ah kumi na moja usiku. Kwa hivyo ikiwa alishughulishwa na usingizi au ugonjwa, basi huswali mchana na kuzifanya shufwa kwa namna ya kwamba huswali Rak´ah kumi na mbili kwa salamu sita. Basi vivyo hivyo na asiyekuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ikiwa atapatwa na mfano wa hilo ambapo akashughulishwa na Witr usiku kwa sababu ya usingizi au ugonjwa, basi aswali mchana. Hata hivyo afanye shufwa na si witiri.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/29382/ما-حكم-قضاء-سنة-الفجر-والوتر
  • Imechapishwa: 02/08/2025