Kila kitu kinawekwa mahali pake. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) alimwambia Muusa na Haaruun (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam):

فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ

“Mwambieni maneno laini huenda akawaidhika au akaogopa.”[1]

Unapojua kuwa upole utamsaidia mtu mjeuri anayesema:

أنا ربكم الأعلى

“Mimi ndiye Mola wenu mkuu!”[2]

na pengine akafanya kiburi na jeuri, anahitaji kukabiliwa kwa upole. Mara nyingine hakuna kinachosaidia isipokuwa ukali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) alitumia yote mawili ukali na upole. Mara nyingi alitumia upole, mara zingine inatokea akakataza maovu kwa mkono wake mwenyewe. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) alimuona bedui amevaa pete ya dhahabu mkononi mwake, akamvua nayo, akaitupa na kusema: “Je, mmoja wenu anakusudia kuweka kaa la moto mkononi mwake?”[3]

Kwa hivyo hali ya msimamo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulikuwa unatofautiana. Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Siku moja nilipokuwa nikitembea na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na alikuwa amejaa joho ya Najraan yenye kingo kali, bedui mmoja akamuwahi na akamvuta joho lake kwa nguvu. Nikatazama shingo yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuona namna ambavo jinsi ukingo wa juu ulivyoiweka alama kutokana na kumvuta kwkae kwa nguvu. Kisha akasema: “Ee Muhammad! Nipeni sehemu katika mali ya Allaah ulionayo! Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamgeukia na akaanza kucheka, kisha akaamrisha apewe zawadi.”[4]

Mara nyingine (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anajibu kwa ukali. Kwa mfano alimwambia Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh):

“Je, wewe ni mfitini mkubwa, ee Mu´aadh?”[5]

Alisema kumwambia Abu Dharr:

“Hakika wewe ni mtu una chembechembe za kipindi kabla ya kuja Uislamu.”[6]

Amesema tena:

“Sidhani kuwa fulani na fulani wanatambua katika dini yetu chochote.”[7]

Kwa hivyo mtu anatakiwa kukiweka kila kitu mahali pake.

[1] 20:44

[2] 79:24

[3] Muslim, Ibn Hibbaan, at-Twabaraaniy na Ibn-ud-Diybaajiy.

[4] Muslim (1057).

[5] Ahmad (3/299), al-Bukhaariy (705) na Muslim (465).

[6] al-Bukhaariy (30) na Muslim (1661).

[7] al-Bukhaariy (6067).

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Mu´aanid, uk. 270-271
  • Imechapishwa: 13/04/2025