Uharamu wa ribaa kwa hali zote bila kujali hekima

Swali: Kwa kuchunguza Aayah za ribaa katika Qur-aan Tukufu inaonekana kwamba mwenye mtaji ndiye anayenufaika na ndiye mwenye manufaa peke yake, na masikini ndiye anayepata madhara na ndiye anayedhulumiwa. Ama miamala ya kibenki iliyopo leo katika benki, anayenufaika ni mwenye mtaji mdogo na manufaa yanakuwa ya pande mbili. Kwa hivyo inatofautiana na ribaa, bali ni kinyume cha ribaa. Ni yepi maoni yenu kuhusu hili? Ke, hamuoni ndani yake kurahisisha kwa waislamu na kuondoa uzito kwao?

Jibu: Hapana, hili ni kosa. Huu ni upotoshaji. Anayenufaika ni huyu na yule. Mkopo anaouchukua mtu unaweza kumnufaisha ambapo anajenga nyumba, anaoa, analipa deni lake na anavumilia nyongeza waliyoipa jina la faida. Benki nayo inanufaika, kwa sababu inatumia fedha hizi katika maeneo mengi, katika miamala mingi, katika kununua bidhaa na kubadilisha fedha kwa fedha. Kwa hiyo inanufaika. Anayechukua mkopo anaweza pia kunufaika katika kile alichokopa kwa ajili yake, kama kununua gari analolitumia, kuoa, kujenga, kulipa deni lililomshughulisha na mengineyo. Hivyo huyu na yule wote wanapata manufaa, hata kama baadhi ya watu wa dini anaweza kuwa amelazimika au akawa na haja ya mkopo huo na ile nyongeza wanayoiita faida, lakini bado yeye anapata manufaa na yule pia anapata manufaa, wote wawili wananufaika. Kwa hiyo yule anayetoa fedha na anapewa faida ni mwenye kunufaika, na benki zinanufaika zaidi kwa sababu zinafanya miamala mingi kwa fedha nyingi sana na hupata faida nyingi. Kwa hivyo nazo pia zinanufaika.

Ribaa ni haramu, ni mamoja iwe amenufaika huyu au yule au wote wawili. Ni juu yetu kushikamana na yale aliyoyasema Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na kujiepusha na yale aliyoyaharamisha Allaah na Mtume wake. Ama kuzingatia hekima na kuwepo kwake au kutokuwepo kwake hilo ni jambo jingine. Ikiwa hekima ipo basi ni nuru juu ya nuru. Ikiwa ipo au haijulikani haitudhuru. Hekima katika hili iko wazi, kwa sababu watu wanalegeza katika mambo haya mradi wanatarajia faida hiyo, basi wanatoa fedha nyingi wakitarajia faida hiyo na huenda Allaah akaleta adhabu yake juu yake ambapo zikaharibika mali zake na adhabu ikamshukia mwenye mali. Matokeo yake akafilisika na mali nyingi zikaenda bure bila faida kwa yule aliyeweka mali. Anapata hasara huyu na yule. Kisha hata tukikadiria kwamba alipata faida kubwa na alitaka faida hiyo, basi hili si sababu ya kuruhusu ribaa, bali hili ni miongoni mwa yanayoharamisha ribaa. Ikiwa mtu aliyelazimika anazuiliwa ribaa hali ya kuwa ametenzwa nguvu na anahitaji, basi vipi yule anayelegeza anayetaka nyongeza, anayetaka ziada na anayetaka kujifurahisha kwa nyongeza huku si mwenye dharurah? Huyo anastahiki zaidi kuzuiwa kujihusisha na ribaa.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3397/تحريم-الربا-ليس-مرتبطا-بمعرفة-الحكمة
  • Imechapishwa: 14/09/2026